Leo March 13, 2018 Baraza la habari Tanzania (MCT) limewasilisha maombi katika mahakama ya Afrika mashariki ya kupinga vipengele kadhaa vya sheria ya huduma ya habari vinavyokiuka mkataba wa habari wa jumuiya ya Afrika mashariki.
Kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2017 imefunguliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) , Kituo cha Msaada wa sheria na haki za binadamu (LHRC) na mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC) wakilalamikia ukandamizaji wa uhuru wa habari .
Akizungumza nje ya mahakama mapema leo, katibu wa baraza la habari Tanzania, Kajubi Mukajanga ameipongeza mahakama hiyo kwa hatua ya kupokea na kukubali maombi yao, tayari kwa kuanza utaratibu wa usikilizwaji wa awali.
Amesema kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa April 13, mwaka huu ambapo waleta maombi watapaswa kuleta viapo na baada ya hapo tarehe 14 May wajibu maombi ambao ni upande wa serikali watapaswa kuleta utetezi wao.
Mukajanga na wenzake wanaiomba mahakama hiyo itamke kwamba vipengele hivyo vinakiuka mkataba wa jumuiya ya Afrika mashariki na kuilazimisha serikali kuvifuta kabisa.
Kesi hiyo inasikilizwa na Jopo la majaji wapatao watatu ambao ni Jaji Kiongozi wa mahakama ya jumuiya ya afrika Mashariki Monika Mugenyi, Jaji Fakihi Jundu na Jaji Dkt Fustin Ntezi lyayo