Waokoaji wanakimbizana na saa kutafuta manusura kwenye vifusi zaidi ya saa 48 baada ya tetemeko baya zaidi la ardhi kutokea nchini Morocco katika zaidi ya miongo sita.
Zaidi ya watu 2,800 waliuawa katika maafa ambayo yaliharibu vijiji katika Milima ya Juu ya Atlas.
Mitetemeko ya baada ya tetemeko itaendelea kutikisa Morocco wiki au miezi kadhaa, mtaalamu wa seismolojia ameonya. Remy Mossu, mkurugenzi wa Kituo cha Ulaya-Mediterranean Seismological Centre, aliiambia Sky News kwamba zaidi ya mitetemeko 25 ya baada ya tetemeko tayari imeikumba nchi hiyo tangu tetemeko la ardhi la 6.8 katika Richter.
“Kutakuwa na mitetemeko ya baadaye. Siyo pengine, ni uhakika,” alisema.
Baadhi ya wanakijiji wanasema wanatatizika kupata nafasi ya kutosha kuzika wafu wao kwani mazishi yanaweza kufanyika kando na kazi ya uokoaji.
Wengine wanatayarisha makaburi ya ziada tayari kwa miili zaidi, hata shughuli za uokoaji zikiendelea.
Mfalme wa Morocco Mohammed VI amezishukuru Uhispania, Qatar, Uingereza na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kutuma msaada, huku serikali ya Uingereza ikipanga kutuma wataalam 60 wa utafutaji na uokoaji na mbwa wanne wa upekuzi nchini Morocco.
Uharibifu wa tetemeko hilo unaweza kuchukua miaka kadhaa kurekebishwa, kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu.