Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, leo Mei 7, 2024 amesema Mkoa huo unatarajia kupokea Mwenge wa Uhuru utakaowasili Mei 08, 2024 mkoani humo, utapitia miradi 39 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 479.6 huku ukikimbizwa kwa takribani kilomita 427.78.
RC Chalamila ametoa kauli hiyo leo Mei 07, 2024 Jijini Dar es Salam, alipokuwa akielezea ujio wa mwenge wa Uhuru ukitokea mkoa wa Pwani.
“Mwenge wa Uhuru kesho utakapowasili katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere Terminal 1, utakapoanza kuzunguuka kwenye Wilaya zote za mkoa huu, Utazindua, Kukagua na kuweka jiwe la msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo” amesema RC Chalamila.
Sanjari na kauli hiyo mkuu wa Mkoa Albert Chalamila ametoa wito kwa Wananchi Dar es Salaam kujitokeza ili kuulaki mwenge wa uhuru kwenye maeneo ambayo utapita ila kukagua miradi na kuzindua.
Mwenge wa Uhuru mwaka huu wa 2024, umebeba kauli mbiu inayolenga kutoa elimu kwa Wananchi kuhusu “Uhifadhi wa mazingira na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa” vilevile ujumbe wa Kudumu wa Mbio za Mwenge katika mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi, Malaria, Dawa za Kulevya, Lishe pamoja na Rushwa.