Leo April 9, 2018 Jalada la kesi inayowakabili vigogo wawili wa uthaminishaji wa madini ya almasi wa serikali, akiwemo Mkurugenzi wa Uthaminishaji Almasi na Vito Tanzania (TANSORT), Archard Kalugendo, bado liko kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Hayo yameelezwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mawakili wa Serikali, Salim Msemo na Emmanuel Majigo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbrad Mashauri.
Kalugendo na mthamini almasi wa serikali, Edward Rweyemamu, walipanda kizimbani mahakamani hapo wakati shauri lilipoitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Msemo amedai jalada hilo ambalo awali lilikuwa kwa DPP lilirudishwa kwa DCI ambaye ameshalifanyia kazi na kurudishwa kwa DPP, hivyo wanasubiri maelekezo ya DPP ili kesi iendelee.
Hata hivyo, Upande wa utetezi umedai hoja hizo wanaona zinazidi kuchelewesha kesi, hivyo upande wa jamhuri useme kwa nini amri halali ya mahakama haitekelezeki.
Wakili Msemo amedai kukamilika kwa upelelezi hakuondoi yale yanayojitokeza na kustahili kufanyiwa kazi katika shauri hilo.
Hakimu Mashauri amesema Hakimu Mwijage amehamishwa kituo cha kazi hataweza kuja kusikiliza tena shauri hilo, ambalo kuanzia sasa limehamia kwake.
Kuhusu ucheleweshwaji wa kesi, Hakimu Mashauri amesema upande wa jamhuri umeeleza hatua kwa hatua, hivyo ameahirisha shauri hilo hadi April 23, 2018, kwa kutajwa na washiakiwa walirudishwa mahabusu.
Washitakiwa hao ambao wanasota mahabusu kutokana na DPP kuzuia dhamana zao, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wakidaiwa kuisababishia serikali hasara ya sh. Bilioni 2.4.