Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema baada ya maandamano makubwa ya Majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha sasa wanaingia katika hatua ya pili itakayohusisha ‘Wiki ya Maandamano’ ambayo itafanyika katika Makao Makuu ya Mikoa yote Tanzania nzima yatakayoanza April 22 hadi April 30, 2024.
Akitangaza Maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama hicho wakati akisoma Azimio la Mtwara akiwa Mkoani Mtwara leo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema “Kamati Kuu yetu inaheshimu kwamba Wakristo wapo kwenye Kwaresma na Waislamu hivi karibuni wataanza mfungo wa Ramadhan, tumesogeza mwezi mzima mbele ili turuhusu wenye imani zao wote wamalize mifungo yao Ibada ili tujumuike kwa pamoja kuandamana”
“Kwakuwa tulitoa wito kwa Serikali kuleta mpango mkakati wa kupunguza gharama za maisha na wameshindwa, Kamati Kuu imejiridhisha kwamba CCM haina mbinu, utashi wala dhamira ya kupunguza gharama za maisha ya Wananchi, kwahiyo sisi kama Chama pamoja na kuwa hatupo Serikalini, tuna uwezo wa kufikiri, kubuni na kutafiti, kwahiyo Kamati Kuu imeielekeza Kamati ya Wataalamu wa Chama kuandaa mpango wa Taifa wa kunusuru Wananchi na gharama za maisha, kupunguza bei za bidhaa na huduma muhimu na mzigo mkubwa wa maisha magumu unaowakabili Wananchi wote”