Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amewasihi Viongozi na Wafuasi wa CHADEMA kudumisha umoja ili uchaguzi ndani ya Chama hicho umalizike salama ukiwemo uchaguzi wa Baraza la Wazee na wa Baraza la Vijana (BAVICHA).
Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) leo January 13,2025, Mbowe amesema “Leo ni siku muhimu sana kwa CHADEMA tunapofanya uchaguzi wetu wa ndani kwa ajili ya Mabaraza ya Wazee na Vijana, napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Wagombea wote wanaoshiriki, kila mmoja wenu ni wa thamani kwetu katika kupigania maono ya Chama chetu”
“Katika safari yetu hii, hebu tukumbuke kwamba uchaguzi huu ni zaidi ya nafasi; ni kuhusu kuunda
mustakabali mzuri kwa CHADEMA na kwa Taifa letu, sote tuna jukumu la kuilinda Taasisi yetu na kuhakikisha tunamaliza hatua hii tukiwa imara zaidi”
“Ninawahimiza wanachama na Wafuasi wote kufuatilia mchakato huu wa kidemokrasia ndani ya
Chama chao, pamoja tukiwa na umoja, tutaweza kufanikisha mambo makubwa, tunaposhirikiana, tunaweza kujenga CHADEMA yenye nguvu zaidi kwasababu yeyote atakayechaguliwa, CHADEMA imeshinda!, Mungu atutangulie katika safari hii”