Makumi ya mbu waliobadilishwa vinasaba (GMO) wameachiliwa nchini Djibouti katika juhudi za kukomesha kuenea kwa spishi vamizi wanaosambaza malaria.
Mbu dume wasiouma aina ya Anopheles stephensi mbu waliotengenezwa na Oxitec, kampuni ya teknolojia ya kibayoteknolojia yenye makao yake makuu nchini Uingereza, hubeba jeni inayoua watoto wa kike kabla ya kukomaa.
Mbu jike pekee ndio wanaouma na kusambaza malaria na magonjwa mengine ya virusi.
Ni mara ya kwanza kwa mbu wa aina hiyo kutolewa Afrika Mashariki na mara ya pili barani humo.
Teknolojia kama hiyo imetumika kwa mafanikio nchini Brazil, Visiwa vya Cayman, Panama, na India, kulingana na Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC).
Zaidi ya mbu kama hao bilioni moja wameachiliwa kote ulimwenguni tangu 2019, CDC inasema.
Kundi la kwanza la mbu hao waliachiliwa hewani siku ya Alhamisi huko Ambouli, kitongoji cha jiji la Djibouti.
Hii ni hatua ya majaribio katika ushirikiano kati ya Oxitec Ltd, serikali ya Djibouti na shirika lisilo la kiserikali la Mutualis.