Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mkoani Morogoro Mhe Salim Alaudin Hasham ameiomba kamati ya mfuko wa jimbo kuelekeza nguvu kubwa katika Ujenzi wa Mabweni katika shule za sekondari ili kupunguza tatizo la mimba za utotoni kwa watoto wa kike ambao wanaishi maeneo ya mbali na shule zao katika jimbo hilo.
Mbunge Salim amependekeza kukarabatiwa kwa Bweni la Shule ya Sekondari Mwaya iliyopo kata ya Ruaha kwani shule hiyo ina wanafunzi wengi wanaotoka mbali na haina bweni kabisa na ni moja ya ahadi yake aliyoahidi kipindi cha kampeni kuwa ataitatua.
Ombi hilo la mbunge linakuja ikiwa ni takribani miaka 5 tangu lilipojengwa bweni na halikukamilika hivyo kuwa boma kwa muda mrefu ikiwa bado adha ya watoto kutembea umbali mrefu inaendelea kuwatesha kila siku.
Wajumbe wa kamati hiyo walimuunga mkono mbunge kwa wazo zuri kwani changamoto hiyo imekuwa kikwazo cha muda mrefu kwa wanafunzi kushindwa kumaliza masomo yao kutokana na mimba za utoto na utoro uliokithiri unaosababishwa na wanafunzi kuchoka kutembea zaidi ya kilometa 10 kutoka wanapoishi mpaka shuleni kwao.
Jumla ya Milioni hamsini (50) zimeelekezwa katika ukarabati wa bweni hilo huku fedha nyengine zikielekezwa katika changamoto nyengine kama Ukarabati wa jiko la hospitali ya wilaya Milioni tano (5), Ukarabati wa madarasa mawili shule ya msingi msogezi Milioni (5), Ukarabati wa chumba cha X-Ray mashine katika hospitali ya wilaya Milioni kumi na sita (16) na Umaliziaji wa nyumba za walimu shule ya sekondari chikuti milioni kumi na tatu (13).
Kwa mwaka huu wa 2022/23 jimbo la Ulanga limepokea kiasi cha shilingi Milioni themanini na tisa laki moja na arobaini (89,140,000/=) ikiwa ni ongezeko la zaidi ya milioni 20 tofauti na mwaka 2021/22 ambapo jimbo hilo limepokea milioni sitini na tano pekee (65,000,000).