Mbunge wa Jimbo la Morogoro mjini Mhe.Dokta Abdulazizi Abood ametoa msaada wa Vifaa Tiba vyenye thamani ya zaidi ya Mil. 28 katika zahanati na vituo vya afya mbalimbali katika Jimbo hilo kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za afya.
Dokta Abood amesema amekua akifanya hivyo mara kwa mara ili kupunguza na kuondoa kabisa changamoto ya kukosa baadhi ya vipimo kwenye baadhi ya Zahanati wakati wa kutoa huduma hiyo kwa wananchi kwa sababu ya kukosekana Mashine za vipimo vya baadhi ya magonjwa yanayowasumbua wananchi.
Mbunge huyo ametoa Vifaa Tiba hivyo katika Kata tano zilizopo kwenye Jimbo hilo wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua maendeleo ya Zahanati ya Mbete na Towero zilipo kata ya Mlimani, Zahanati ya Kibwe Kata ya Boma, Zahanati ya Uwanja wa Taifa iliyopo Kata ya Uwanja wa Taifa, Zahanati ya Konga iliyopo Kata ya Mzinga pamoja na Kituo cha Afya cha Sina kilichopo Kata ya Mafisa.
Vifaa vilivyotolewa kwenye ziara hiyo ni pamoja na Vitanda vya huduma ya kwanza vitatu (3), Vitanda vya kusaidia Kinamama wajawazito kujifungua (Derivery Bed) 3, Hadubini (Microscope Tube) 4, Sentrifyugi Mashine 5 pamoja na Mashine maalum ya kumsaidia mgonjwa kupumua haswa Kinamama wajawazito, Mashine 1 na Vifaa vinginevyo kama vile Glucose Mashine 5, ambavyo kwa ujumla wake vifaa hivyo vimegharimu kiasi cha zaidi ya Tsh. Mil. 28 zilizotoka mfukoni mwa Mbunge huyo ili kurahisisha na kuboresha huduma za Afya kwa wananchi wa Jimbo hilo.
Aidha, Mbunge huyo amebainisha kuwa, lengo kuu la kupeleka Vifaa hivyo ni kutaka kuona wananchi wa Jimbo hilo wanapata huduma safi za Kiafya ili wawe chachu ya kulijenga Taifa la Tanzania, hivyo amewataka wataalamu wa Afya kuvitumia kikamilifu kwa kuleta matokeo chanya, ambapo atoa Wito kwa wananchi katika maeneo tofauti kutumia Zahanati hizo pamoja na vituo vya Afya vya Serikali ili kuonesha kuwa uwekezaji huo wa Vifaa unakuwa na tija kwenye utoaji wa huduma za Afya ndani ya Jimbo hilo.
Dokta Abood amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amekua akitoa fedha nyingi katika kujenga vituo vya afya,zahanati na hospitali hivyo amemuunga Mkono kwa vitendo katika uboreshaji wa huduma za afya
Katika hatua nyingine, Dokta Abood ametimiza ahadi ya Mifuko 45 ya saruji katika Mitaa ya Kikundi, Kisosa na Chalagule na Chepe 5 katika Kata ya Mlimani kufuatia maombi ya wananchi wa Kata hiyo wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika hivi karibuni Mwaka huu, ambapo Mbunge aliahidi kusaidia vifaa hivyo ili kurekebisha na kujenga Vivuko katika Mitaa tajwa na kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali.
Naye Diwani wa Kata ya Mlimani iliyopo katika Jimbo hilo Mhe. Zinduna Kombo amesema kwamba Chama tawala kinatekeleza Ilani kwa vitendo kuanzia kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusogeza huduma za Afya kwa wananchi kwa kujenga Hospitali, Vituo vya Afya pamoja na Zahanati, ambapo kwa upande wa Jimbo la Morogoro Mjini Mhe. Abood ameamua kujitoa ili kusaidia vifaa tiba kwa lengo la kuunga Mkono jitihada za Rais.