Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi, Dkt. David Mathayo, amekabidhi mchango wa mifuko 500 ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Msikiti wa Hedaru.
Hatua hii ni sehemu ya jitihada za kusaidia waumini wa dini ya Kiislamu kukamilisha msikiti huo ili kuwa na sehemu bora ya kuswalia.
Dkt. Mathayo alitoa msaada huo kupitia fedha taslimu shilingi milioni nane, akitimiza ahadi aliyotoa awali alipoalikwa kutembelea eneo la ujenzi wa msikiti huo. Mchango huo ulitolewa katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wananchi wa kata hiyo.
Akikabidhi msaada huo dkt Mathayo alisema yeye kama mbunge Hana upendeleo wa dini kwa kuwa wote ni wapiga kura wake.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Imamu wa Msikiti Mkuu wa Hedaru shekh Abbas alishukuru kwa mchango huo muhimu na kuahidi kuwa saruji hiyo itatumika ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa.
Imamu Abbas bin khalid amemshukuru mheshimiwa Mathayo ambapo yeye na waumini wengine wametumia fursa hiyo kumuombea dua ili Mwenyeezi Mungu ampe afya njema na aweze kutimiza mahitaji yake ipasavyo.
Mbali na msaada kwa msikiti, mbunge Mathayo pia alikabidhi mifuko mingine 200 ya saruji kwa shughuli mbalimbali za maendeleo katika kata hiyo.
Aidha, alitoa viti 250 kwa vikundi vya kina mama pamoja na fedha taslimu kwa ajili ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.
Mchango huu unaendelea kuonyesha dhamira ya mbunge huyo katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Jimbo la Same Magharibi.