Mbunge wa jimbo la Njombe Mjini Deo Mwanyika ametoa mitungi ya gesi kwa baba lishe na mama lishe wanaofanya kazi kwenye kituo cha mabasi cha Njombe mjini kilichopo kwenye kata ya Mji Mwema.
Mwanyika ametoa mitungi kwa makundi hayo akiwa na lengo la kuendelea kuiunga mkono serikali katika jitihada za kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi pamoja na kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa ambao umekuwa ukisababisha madhara kwa watumiaji.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi mitungi hiyo Mbunge Mwanyika amesema anatamani kuona baba lise na mama lishe wanakuwa chachu ya utunzaji wa mazingira kwa kuingia kwenye matumizi ya gesi kuliko kuendelea kuharibu mazingira kwa kutumia kuni pamoja na mkaa.
“Nia yetu ni kutaka muendelee kutumia gesi wakati wa kuandaa vyakula na matumizi mengine,tuache kukata kuni na kuchoma mkaa hasa maeneo ya mjini na zoezi hili litakuwa ni endelevu kwenye maeneo mengine”amesema Mwanyika
Happy Msango ni mwenyekiti wa mama lishe na baba lishe wa kituo hicho cha mabasi,kwa niaba ya wajasiriamali hao ametoa shukrani kwa msaada huo huku pia wakiomba kurekebishiwa changamoto ya miundombinu ya jengo lao linalotumiwa wakati wa kuandaa chakula ikiwemo urekebishwaji wa sakafu ambapo Mwanyika ametoa ahadi ya kushirikiana na halmashauri ili kufanya marekebisho hayo.