Mbunge Tauhida Cassian Gallos, amechangia maelezo ya Serikali kuhusu mapendekezo ya kuridhia mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa Bandari Tanzania.
“Kwa mara ya kwanza nikiwa ndani ya Bunge lako Tukufu, nikishuhudia Mkataba huu ukija kwa uwazi zaidi. Ifike wakati kama Watanzania tutambue wapi tunatoka na wapi tunakwenda. Namna ambavyo mkataba huu umeletwa ndani ya Bunge ni makubaliano ya wazi yasiyojificha.” Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos, Mbunge
“Kuna maneno yanayozungumzwa kwamba huu ni Mkataba. Watanzania ifikie mahali tuamke. Tujue hizi kelele zinatoka wapi. Hakuna vita vikubwa duniani kama vita vya uchumi.”Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos Mbunge.
“Wakati huu tuliokuwa nao ukimuona Mtanzania hususan mwenye uongozi anayeongoza watu anatamka kauli ya ubaguzi tunamshangaa sana. Mimi hapa baba yangu ni mtu wa Songea, mama yangu ni Mzaramo. Mimi pia nimezaliwa Zanzibar na Mbunge kutoka Zanzibar. Leo tukisimama Watanzania tunaanza kubaguana hatutofika.”Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos Mbunge.
“Serikali yetu haikatai kukosolewa. Makosa ambayo tunayakosoa inafanya uboreshaji zaidi. Nilitegemea kiongozi anayeongoza watu anahubiri amani na umoja na mshikamano. Leo nashangaa kiongozi wa siasa anapoleta ubaguzi ndani ya chama chake Naibu Katibu Mkuu anayetoka Zanzibar anajifikiria vipi.”Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos Mbunge.
“Tunataka Wabunge tufike wakati tutamani kumuona mtu anayetoka hapa ndani ya jengo hili anakuwa pia ni Rais wa Zanzibar kutoka Bara. Tuipelekeni Tanzania huko. Tuionyesheni Katiba yetu na kuiboresha na kuhakikisha Tanzania inakuwa moja. Watu wa Tanzania wanakuwa wamoja. Itikikadi za kisiasa tusivunje Tanzania.”Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos Mbunge.