Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Peter Cherehani ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufuatia na hatua iliyochukuliwa ya kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi na kurejesha eneo la pori hilo kwa wananchi hatua mabayo itawawezesha kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo Ufugaji na Uvuvi.
Cherehani ameyasema hayo Jimboni kwake Ushetu katika mkutano wa hadhara uliofanyika mbele ya wananchi ambapo amesema kuwa suala hilo lilipelekea kuwapo kwa changamoto za migogoro ya ardhi baina ya Serikali na Wananchi waishio katika maeneo hayo na kuongeza kuwa hatua hiyo imeongeza imani ya wananchi kwa serikali yao.
Itakumbukwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi imesababisha kukosekana kwa fursa za kiuchumi kwa wananchi kutokana na kuzuia kufanyika kwa shughuli za kibinadamu ambapo Serikali iliona ni vyema kufuta Hifadhi hiyo na kuwapa fursa wananchi kufanya shughuli za kibinadamu baada ya sheria ya misitu sura namba 323 inayoruhusu kufanyika kwa shughuli za kiuchumi ndani ya Hifadhi za Misitu kwa kuzingatia matakwa ya uhifadhi na utaratibu maalum.
Mbali na hivyo Mheshimiwa Cherehani ameipongeza Serikali katika juhudi zake za kuwaletea wananchi wa Jimbo la Ushetu maendeleo makubwa kama vile ujenzi wa barabara za lami, miundombinu ya umeme, kuondoa kodi za manunuzi ya tumbaku pamoja na mradi wa maji wa Ziwa Victoria.