Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Peter Cherehani ni miongoni mwa wabunge waliosimama kuchangia hoja ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.
Mhe. Cherehani amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja kama Mbunge wa Jimbo la Ushetu, tayari wameshapokea kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 17 za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo na kumpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika juhudi anazozifanya za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha Mhe. Cherehani amezungumzia changamoto ya kukatika kwa umeme katika mji wa Kahama pamoja na Halmashauri zake za Ushetu na Msalala ambapo kuna mkandarasi mmoja tu ambaye anasimamia miundombinu ya umeme katika Halmashauri tatu.
Mbali na changamoto ya umeme pia Mhe. Cherehani amezungumzia adha ya usafiri wanayokumbana nayo wakazi wa jimbo la Ushetu inayotokana na ubovu wa miundombinu ya barabara na kumuomba Waziri wa Ujenzi akashuhudie changamoto wanayopitia wananchi wa Ushetu katika miundombinu ya usafiri.