Leo May 28, 2018 Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe ameijia juu ofisi ya Bunge la Tanzania kwa kusema kuwa urafiki wao na wabunge wa upinzani ni wamashaka.
Amesema kuwa kitendo cha Ofisi ya Spika wa bunge kutoa taarifa ya mazishi ya Mbunge wa Buyungu mkoani Kigoma, Kasuku Bilago kabla ya kufanya mawasiliano na viongozi wa chama kimewashtua sana.
“Bilago alifariki jumamosi mchana, saa kumi jioni ofisi ya bunge imetangaza taratibu za mazishi wakati tuko katika harakati za kuhifadhi mwili, hatujakaa kikao, hatujawasiliana na ndugu, huyu ni kiongozi wa mikoa mitatu na Mbunge”.
“Pasipo mazungumzo ofisi inatoa taarifa ya mazishi hilo jambo limetuhuzunisha sana. Wamesema Bilago aagwe leo kama wangekuwa wanampenda wangemtibu kwanza,” amesema Mbowe
Mbowe amesema Bunge la Jamhuri ya Muungano limeundwa na sehemu Kuu mbili ambazo ni serikali (CCM) na upinzani.
“Upande wa pili huu wa bunge popote wanapofikia kufanya maamuzi tunaona maamuzi yao hayana nia njema kama walikuwa wanampenda sana wangetibia,” amesema.
Hata hivyo Mbowe amesema Bunge lilitaka Bilago aagwe bungeni leo May 28, 2018 lakini baada ya chama kukaa na familia imeamua kesho ndio iwe siku ya kuagwa bungeni Dodoma na kisha mazishi yatafanyika siku ya Alhamis mkoani Kigoma.
Bilago alizaliwa Tarehe 2/2/1964 na amefariki akiwa Mbunge wa kuchaguliwa wa jimbo la Buyungu ambapo alichaguliwa mwaka 2015.