Mwanasoka wa Italia Salvatore Schillaci almaarufu “Toto” ambaye aliibuka kuwa shujaa wa Kombe la Dunia mwaka 1990, amefariki dunia kwa ugonjwa wa saratani ya utumbo.
Mshambuliaji huyo alifunga magoli sita katika ardhi ya kwao katika Kombe la Dunia 1990, vilevile alipata tuzo ya Mfungaji Bora na tuzo ya mchezaji bora kwa ujumla.
Schillaci amewahi kuzichezea timu mbalimbali ikiwemo Juventus na Inter Milan, na kustaafu mwaka 1999.
Kupitia Mtandao wa X, Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni amempa heshima Schillaci kwa kuandika “ishara ya soka inatuacha,mtu aliyeingia kwenye mioyo ya Waitaliano na Mashabiki wa michezo duniani kote”
”Asante kwa hisia ulizotupa, kwa kututimizia ndoto, shangwe na kuipeperusha bendera yetu, kwaheri bingwa”
Rais wa Shirikisho la soka la Italia Gabriele Gravina ametangaza kuwepo kwa dakika 1 ya ukimya kwa kumkumbuka Schillaci kabla ya mechi zote zitakazochezwa nchini humo ndani ya wiki hii.