Mchungaji Theo Ebonyi wa Faith on the Rock Ministry International amekashifu machapisho yanayosambazwa kwenye vyombo vya habari akidai kwamba alikamatwa na EFCC.
Kulingana na taarifa mchungaji huyo alizuiliwa na kuachiliwa kwa dhamana mwaka jana, lakini hili limetolewa tu kwa umma, msemaji wa mamlaka ya kupambana na ufisadi amenukuliwa akisema.
Bw Ebonyi alisema habari hizo ni habari “feki” zinazoenezwa na wanablogu.
Hakuzungumzia tuhuma zinazomkabili.
Tume ya Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha ya Nigeria (EFCC) inadai Bw Ebonyi aliwataka waathiriwa wake kulipa ada ya $1,300 kila mmoja ili kupata ruzuku ya $20bn kutoka kwa Wakfu wa Ford wenye makao yake Marekani.
Walakini, inasema kwamba wakfu huo haukutoa ruzuku kama hiyo.
“Uchunguzi wa EFCC ulionyesha kuwa Ford Foundation haikuwa na mpangilio, ruzuku, uhusiano au biashara na Ebonyi,”shirika hilo lilisema katika taarifa.
“Wakfu huo ulijetenga naye pamoja na shirika moja lisilo la kiserikali ikisisitiza kuwa haina uhusiano wowote nao.”
EFCC pia inadai kuwa Bw Ebonyi, ambaye anasimamia kanisa la Faith on the Rock Ministry International, alitumia pesa zilizopatikana kwa njia ya udanganyifu kununua mali yake.
Anatazamiwa kushtakiwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika, EFCC inasema. Bado haijafahamika ni mashtaka gani haswa atakabiliwa nayo.