Mchungaji Ezekiel Odero wa kanisa la New Life Prayer Center ambaye alishukiwa kuwa mhusika mkuu wa mauaji ya Shakahola hatimye aliondolewa mashtaka hayo.
Odero aliachiliwa kuwa huru na mahakama ya Shanzu huko Kilifi huku hakimu akiamuru,mchungaji huyo kurudishiwa dhamana ya Sh milioni 1.5.
Timu ya mashtaka iliyokuwa ikiongozwa na Antony Musyoka, iliambia vyombo vya usalama vilivyokuwa vikifanya uchunguzi kuwa hawakupata ushahidi wowote unaomhusisha Odero na kanisa lake na kasisi Paul Mackenzie.
“Tunaonelea kwamba jalada hilo lifungwe katika hatua hii kwa kuwa upelelezi umekamilika na mapendekezo yamo katika majalada ya polisi ambayo yametumwa kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ,” alisema.
Kikao cha kusikilizwa kwa kesi hiyo kilichoongozwa na Hakimu Mkuu Joe Omido kilifikia tamati baada ya Hakimui kutoa uamuzi kwamba Odero aachiliwe huru na kwamba dhamana ya pesa taslimu Sh milioni 1.5 ambayo mhubiri huyo alilipa mapema kortini kwa kuachiliwa kwake kwa muda irudishwe.