Mawakili Sheck Mfinanga na John Mallya ambao wanamwakilisha Mbunge wa jimbo la Arusha mjini, Godbless Lema katika kesi ya kudaiwa kumdhalilisha Rais John Magufuli wamepinga vielelezo vilivyowasilishwa Mahakamani na upande wa jamhuri kwa madai kwamba vimeokotwa mtaani.
Mawakili hao wamepinga vielelezo hivyo ambavyo ni kanda za video zinazomwonyesha Lema akiwa katika eneo la mkutano mnamo October 22 mwaka juzi katika eneo la Kambi ya Fisi jijini Arusha akitamka maneno yanayodaiwa kumdhalilisha Rais Magufuli .
Vielelezo hivyo vilivyowasilishwa jana na shahidi wa sita upande wa jamhuri, Inspekta Aristides(44) ambaye ni Afisa wa polisi idara ya uchunguzi na kisayansi Makao Makuu ya Upelelezi jijini Dar es salaam.
Shahidi huyo ambaye ni mchunguzi wa picha za video na sauti alifika mbele ya Mahakama hiyo na kuwasilisha vielelezo vyake na kusema kwamba mnamo November 21 mwaka juzi akiwa ofisini kwake alipokea kanda za video aina ya Sony kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Arusha vikiwa vimefungwa kwenye bahasha.
Akijibu swali lililoulizwa na wakili wa upande wa Jamhuri Agnes Hyera kwamba ana maoni gani kuhusu vielelezo hivyo shahidi huyo aliiomba Mahakama hiyo ipokee vielelezo hivyo kama ushahidi katika kesi hiyo.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, Devotha Msofe wakili wa upande wa utetezi Mallya alipinga uwasilishwaji wa vielelezo hivyo kwamba una mapungufu ya kisheria kwa kuwa shahidi huyo sio yeye aliyerekodi kanda hizo na hivyo hakustahili kuuwasilisha mbele ya Mahakama hiyo.
Akiunga mkono hoja ya Mallya wakili upande wa utetezi Mfinanga aliiambia Mahakama hiyo kwamba shahidi huyo alitumiwa kanda hizo akiwa jijini Dar es salaam na kimsingi hastahili kusimulia kitu ambacho hajakiona.
Mara baada ya hoja hizo Hakimu Msofe amehairisha kesi hiyo hadi February 16, 2018 ambapo anatarajia kutoa uamuzi kuhusu endapo vielelezo hivyo vinastahili kupokelewa na Mahakama kama ushahidi au la.
VIDEO: “NABII TITO” AMWAMBIA KAMANDA “MIMI NINATUMIA BIBLIA”