Aliyekuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bernard Kamilius Membe hii leo July 16 ametangazwa rasmi kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo yeye na familia yake ambapo baada ya kukaribishwa amezungumza yafuatayo.
“Kiongozi wangu Zitto Kabwe wewe ni mfano wa vijana na ninashukuru vijana wadogo kama kina Nondo unawalea, toka tulipokutana miaka ya 2000 ukiwa na Mama yako mzazi, wewe unapenda binadamu na kuheshimu wenzako, Mungu na Malaika wako na wewe”
“Naomba nitoe wito kwa kambi yote ya upinzani, ni lazima tuungane, uchaguzi ni wetu mimi naomba kabisa tuungane vyama vyote kama walivyofanya TLP na Cheyo kuwaunga mkono wenzetu, tuungane, umoja ni nguvu””Mkoa wangu wa Lindi na Mtwara hivi sasa wanasubiri kuhamia ACT hivi ninavyozungumza nina wanachama wa CCM wanataka wajiunge, lakini jumla yake tuna kadi zaidi ya Elfu nane zitakazomiminika kwangu ili nizirudishe CCM”
“CCM na ujanja wetu huko nyuma hatukumshinda Maalim Seif, Pemba hawawezi kuichukua na hawatoichukua na Maalim ni mjanja katika siasa hizi, kwahiyo tuko hapa na Rais mpya wa Zanzibar nasema sifa hizi wala si kwa kujipendekeza”
“Tukipata nafasi tutalishughulikia suala la ajira kwa vijana, tutapandisha mishahara ya wafanyakazi na kwenye utawala wa ACT hakutakuwa na hofu yoyote, nimejiunga ili kushawishi wananchi kuleta mabadiliko, ACT ni chama ambacho kinakuwa kwa kasi sana kupita vyama vyote”
“Ninawaomba ACT tukiingia madarakani tuurudishe mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, tuendeleze mradi wa Gesi wa Mtwara na Lindi na bei nzuri ya Korosho, Mbaazi na Ufuta lazima tuwe nayo, Mimi kule nimefukuzwa tena kwa aibu na fedheha na Vijana ambao ningeweza kuwazaa, na sikufanya kosa lolote, kosa ni kugombea Urais 2015, na kuonesha nia 2020 ya kugombea, sasa Mtu anaposema wee Mzee utarudi ulikotoka kama yule mwenzako, nirudi wapi?”