Mfalme Charles wa tatu wa Uingereza alifanya kikao cha faragha na familia ya mpiganiaji uhuru wa vita vya Mau Mau nchini Kenya aliyeuwawa Dedan Kimathi.
Alifanya ziara hiyo siku moja baada ya mfalme huyo kuelezea kile alichokiita “masikitiko na majuto makubwa” ya yaliyotokea enzi za ukoloni.
Ubalozi wa Uingereza umesema mkutano huo ulikuwa fursa ya mfalme Charles kusikia moja kwa moja kuhusiana na madhila waliyofanyiwa Wakenya wakati walipokuwa wakipigania uhuru. Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni mwenyekiti wa Chama cha Wakongwe wa Mau Mau.
Mfalme Charles na mkewe Carmilla ambao wako nchini Kenya kwa ziara ya siku nne, hajaomba radhi kuhusiana na yaliyotendwa na Uingereza katika kipindi cha ukoloni nchini humo, kama ilivyotarajiwa na Wakenya wengi.