Kwa mara ya kwanza katika miongo saba, Mtawala wa Uingereza ametawazwa rasmi baada ya Askofu Mkuu wa jimbo la Canterbury Justin Welby kuliweka Taji la Mtakatifu Edward juu ya kichwa cha Charles III, sehemu muhimu zaidi kwenye ibada ya kutawazwa.
Mfalme Charles amekuwa mtawala wa 40 kutawazwa katika tafrija takatifu iliyofanyika katika Kanisa la Westminster Abbey, tangu mtawala “William the Conqueror” alipopakwa mafuta na kuwa Mfalme wa Uingereza ndani ya Kasri lake Siku ya Krismasi mwaka 1066.
Mfalme huyo aliyetawazwa hivi karibuni atavaa Taji lake katika Jimbo la Kifalme kwa mara ya kwanza na kuvaa vazi la kifahari lenye rangi ya zambarau katika sherehe rasmi. Kabla ya Mfalme kutawazwa, Dean wa Westminster alileta taji kwa Askofu Mkuu wa Canterbury ambaye alitoa sala ya baraka.
Miongoni mwa walioalikwa walikuwa washirika wa familia ya Kifalme, waziri mkuu, wawakilishi kutoka mabunge, wakuu wa nchi, na washiriki wengine wa familia ya kifalme kutoka kote ulimwenguni.
Kando na waliohudhuria hafla hiyo, Mamilioni ya watu duniani wamefuatilia sherehe hizo kwa njia ya mitandao, hafla hiyo ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III jijini London imejumuisha dini na tamasha mbalimbali.
Sherehe rasmi ziliaanza kwa msafara kutoka Buckingham Palace hadi Westminster Abbey huku maeneo ya kutazama tukio hilo yakiwa kwenye njia iliyofunguliwa saa kumi na mbili asubuhi kwa saa za Uingereza.
Wanajeshi wengine 1,000 walipanga foleni njiani, Msafara wa mwaka huu umeonekana kuwa madogo zaidi kuliko ule wa mwaka 1953 wakati familia za kifalme na waziri mkuu wa Jumuiya ya Madola walikuwa miongoni mwa washiriki.
Taji alilovishwa Mfalme Charles limetengenezwa kwa dhahabu na limewekewa idadi ya Almasi 2,868, madini ya sapphire 17, Emeralds 11, lulu 269, na madini ya rubi manne. Taji hili ni maarufu kutokana na baadhi ya vito vya thamani vilivyotumika kutengenezea, katika hizi ni pamoja na almasi ya “Cullinan II” ambalo chimbuko lake ni nchini Afrika Kusini na ndio jiwe la Almasi kubwa kuwahi kugunduliwa.