Mfalme Charles III anaanza ziara ya kiserikali nchini Kenya leo Jumanne, ambapo atakabiliwa na matakwa mengi ya kuomba radhi kwa ukoloni wa zamani wa Uingereza katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Ziara hiyo ya siku nne, ambayo inakuja kabla ya Kenya kuadhimisha miaka 60 ya uhuru mwezi Desemba, ni ya kwanza kwake kama mfalme katika nchi ya Jumuiya ya Madola. “Ziara hiyo inatoa ishara kwa ushirikiano thabiti na wenye kudumu kati ya Uingereza na Kenya,” ubalozi wa Uingereza umesema katika taarifa.
Lakini ziara ya Mfalme Charles III, 74, na Malkia Camilla, 76, pia itafanya iwezekane kujadili “mambo mabaya ya historia ya pamoja ya Uingereza na Kenya” katika miaka iliyotangulia uhuru, Kasri la Buckingham Palace limebaini.
Kati ya mwaka 1952 na 1960, zaidi ya watu 10,000 waliuawa nchini Kenya kufuatia uasi wa Mau Mau dhidi ya mamlaka ya kikoloni, mojawapo ya ukandamizaji wa umwagaji damu zaidi wa ufalme wa Uingereza.
Baada ya miaka mingi ya kesi, London ilikubali mwaka 2013 kuwafidia zaidi ya Wakenya 5,000, lakini baadhi wanasubiri mfalme aombe msamaha rasmi kwa hatua za awali za Uingereza.