Mfalme Charles wa tatu, wa Uingereza pamoja na mkewe wake, malkia Camilla watazuru Kenya baadaye mwezi huu katika ziara yao ya kwanza katika nchi mwanachama wa jumauia ya madola, imesema taarifa ya kasri ya Buckingham.
Taarifa ya kasri ya Buckingham imesema ziara yao itaanza Oktoba 31 hadi Novemba 3, kwa lengo la kusherehekea uhusiano na ushirikiano mzuri kati ya nchi hizo mbili.
Aidha taarifa hiyo imesema kwamba mfalme Charles na mkewe Camilla wazuru kaunti za Nairobi, Mombasa na maeneo yaliokaribu.
Ratiba ya ziara yao inalenga kuangazia namna nchi hizo zimekuwa zikifanya kazi kwa pamoja katika masuala tofauti ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, kukuza fursa na ajira kwa vijana pamojana kuhakikisha usalama wa ukanda.
Rais wa Kenya William Ruto alitoa mwaliko kwa mfalme Charles na mkewe kuzuru taifa hilo, wakati huu ikijiandaa kwa maadhimisho ya miaka sitini tangu Kenya ijipatie uhuru kutoka kwa Uingereza.