Mfanyabiashara, Edson Beanga amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akiwa anakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kujifanya kuwa Afisa wa TAKUKURU kinyume cha sheria.
Beanga (37), mkazi wa jijini DSM anefikishwa mahakamani hapo leo Desemba 31, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.
Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon akimsomea mashtaka hayo amedai, Desemba 11 mpaka 15, mwaka huu jijini Dar es Salaam mshtakiwa alijifanya kuwa ni Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na kujitambulisha kwa mtu aliyejulikana kwa jina la Juma said Tandu ambaye ni Mchunguzi wa Takukuru jambo ambalo lilikuwa siyo kweli.
Shtaka la pili ni kughushi, Agosti 4, mwaka 2018 jijini DSM mshtakiwa alitengeneza nyaraka ya uongo ambayo ilikuwa ni fomu iliyokuwa ikionesha kuwa ilitolewa na TAKUKURU jambo ambalo siyo kweli.
Wakili Simon ameendelea kudai, shtaka la tatu ni kughushi ambapo Agosti 4, mwaka 2018 jijini Dar Dar es Salaam mshtakiwa alitengeneza nyaraka ya uongo ambacho kilikuwa ni kitambulisho kikionesha kimetoka NEMC ambapo kilionesha ni cha mtu aitwaye, Boniface Mlema, kwamba kilitolewa na NEMC kumbe ni uongo .
Baada ya kusomwa kwa mashtaka hayo Wakili upande wa Jamhuri amedai upelelezi bado haujakamilika na Hakimu Chaungu ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 14, 2021 kwa kutajwa na mshtakiwa alirudishwa rumande.