Taarifa iliyowasilishwa mahakamani na afisa wa uchunguzi ilisema kwamba kampuni inayomilikiwa na mfanyabiashara Sydney Mfundo Gcaba inadaiwa kutuma zaidi ya rand 800,000 ($42,000; £33,000) kwenye akaunti ya benki ya mmoja wa washukiwa wanaoshtakiwa kwa mauaji ya rapper huyo.
Malipo hayo yanadaiwa kufanywa siku moja baada ya mauaji ya AKA.
Mwendesha mashtaka, akinukuu rekodi za simu, pia alisema kuwa mshukiwa aliyepokea pesa hizo, Mziwethemba Harvey Gwabeni, alidaiwa kupiga simu kwa Bw Gcaba kabla ya shughuli hiyo kukamilika.
Bw Gcaba bado hajatoa maoni yake kuhusu kauli ya mwendesha mashtaka.
Mwendesha mashtaka anadai kuwa pesa hizo ziligawanywa kwa usawa kati ya washukiwa saba.
Bw Gwabeni alisema katika hati ya kiapo kwamba alipokea fedha hizo kama malipo ya huduma za mashauriano alizotoa kwa kampuni hiyo.
Lakini mwendesha mashtaka alidai kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa Bw Gwabeni alitoa huduma yoyote kwa kampuni hiyo ili kuidhinisha malipo hayo.
Bw Gcaba ni mwanachama wa familia yenye nguvu ya Gcaba, ambayo inamiliki himaya ya teksi na biashara nyingine kadhaa katika jimbo la pwani la KwaZulu-Natal na kote Afrika Kusini.