Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, imemfikisha mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Nzega, Dickson Mtandu (52) katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Nzega kwa tuhuma ya kuomba rushwa ya Milioni 1.5 toka kwa mfanyabiashara wa nyumba ya kulala wageni.
Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Wilaya ya Nzega, Mazengo Joseph aliiambia mahakama mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Nzega, Joseph Mwita kuwa mtumishi huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 15 (1)(a)(2) na 3 (a) cha sharia ya kuzuia na kupambana na rushwa Na 11/2007.
Awali, mwendesha mashtaka huyo wa TAKUKURU aliiambia mahakama kuwa kati ya Agosti 8, 2020 na Agosti 28, 2020 kwa nyakati tofauti, mshitakiwa akiwa eneo la Mery Pud mjini Nzega, aliomba rushwa ya Sh milioni 1.5 kutoka kwa Sahani Katuli ili asimchukulie hatua za kisheria kwa kutotoa risiti ya EFD katika nyumba yake ya kulala wageni ya kipozo ilioko mjini Nzega.
Mazengo aliendelea kuiambia mahakama kuwa Agosti 29, 2020 mshitakiwa alikamatwa na maofisa wa Takukuru Wilaya ya Nzega akipokea rushwa ya Sh 400,000 kati ya zile Sh milioni 1.5 alizoomba kutoka kwa mlalamikaji Sahani Katuli baada ya kuwekewa mtego.
Hata hivyo, baada ya kusomewa shitaka mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo ambapo kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 20, 2020 na mshitakiwa yuko nje kwa dhamana ya Milioni moja na wadhamini wawili.