Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli leo January, 2018 amekutana na Mjumbe Maalum wa Rais wa Rwanda na aliyewahi kuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Donald Kaberuka na kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Tanzania na umoja wa Afrika (AU).
Baada ya mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu DSM na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Dkt. Kaberuka amesema uchumi wa Tanzania unakua vizuri na amempongeza Rais Magufuli kwa jinsi anavyosimamia ukuaji wa uchumi huo.
“Nimefurahi sana jinsi Tanzania inavyokwenda mbele, maendeleo yanakwenda kwa kasi na Rais anafahamu kabisa kwamba katika Afrika nchi zetu zinahitaji kuwa na uchumi bora, ningependa kumpongeza na Watanzania wote kwa kazi nzuri wanayofanya” -Dkt. Kaberuka.
Wakati huo huo Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Zimbabwe hapa nchini anayemaliza muda wake Edzai Chimonyo na kumpongeza kwa uwakilishi mzuri alioufanya kwa miaka 10 aliyoiwakilisha Zimbabwe hapa nchini.
Rais Magufuli amemuomba Chimonyo kumfikishia salamu za pongezi Emmerson Mnangagwa kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zimbabwe na amemuhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri wa kihistoria na kidugu uliopo kati yake na Zimbabwe.
“Naomba umwambie Rais Mnangagwa kuwa namkaribisha atembelee Tanzania na namtakia heri katika majukumu yake, natarajia ataendeleza uhusiano na ushirikiano wetu ili tuweze kujiimarisha zaidi kiuchumi kwa manufaa ya nchi hizi mbili” -Rais Magufuli.
Balozi Chimonyo ameshukuru Rais kwa ushirikiano mkubwa alioupata katika kipindi chake cha Ubalozi hapa nchini na amempongeza kwa namna anavyoiongoza nchi, huku akitaja baadhi ya mambo yanayofanywa kwa mafanikio makubwa kuwa ni mapambano dhidi ya rushwa, ujenzi wa miundombinu hususani barabara, madaraja na viwanja vya ndege.
BREAKING: RAIS MAGUFULI AMETENGUA UTEUZI WA MKURUGENZI BUTIAMA