MFUKO wa utamaduni na sanaa umefanikiwa kutoa mikopo ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.077 kwa miradi 45 ya sanaa nchini ili kukuza sanaa na kutimiza azma ya Rais Samia suluhu Hassan ya kutoa mikopo kuwainua wasanii.
Afisa mtendaji mkuu mfuko wa utamaduni na sanaa uliopo chini ya Wizara ya Utamaduni sanaa na michezo Nyakaho Mahemba alisema hayo katika warsha ya kuwajengea uwezo wadau wa utamaduni na sanaa mkoa wa Morogoro iliyofanyika mjini hapa.
Alisema kupitia mwongozo wa mkopo huo uliotolewa na Rais Samia wameweza kutoa mafunzo kwa wadau 6,121 wa sanaa kutoka mikoa 11 ambapo kati yao wanawake wakiwa ni 2,031 na wanaume wakiwa ni 2,721.
Alisema tangu mfuko huo uanze hadi Sasa umeweza kuzalisha ajira 88,755 ikiwemo kuboresha studio 21 ambazo zitasaidia wasanii kutengeneza kazi zao hapa nchini na kuondokana na gharama ya kutafuta huduma nje ya nchi.
Alisema mfuko huo ulianzishwa mwaka 2022 kwa kutoa mikopo kwa wasanii wa Jiji la Dar es salaam ambapo kwa Sasa umeanza kupanuka na kutoa huduma kwa mikoa mbalimbali nchini wakianzia na mkoa wa Morogoro na Wilaya zake.
Aidha alisema lengo la Serikali kupitia mfuko huo kwa kushirikiana na benki za Crdb na Nbc ni kutoa zaidi ya sh bil 20 kwa wadau wa sanaa ili kukuza mitaji na kuongeza vipato vyao sambamba na kukuza uchangiaji wao katika pato la Taifa.
Naye Meneja bidhaa na huduma kutoka Benki ya NBC makao makuu Jonathan Bitababaje alisema watahakikisha wanatoa elimu ya namna na wakati sahihi wa kukopa kwa wadau wa sanaa huku wakiwasisitiza kukidhi vigezo ndipo wapate mikopo inayostahili ili kujikwamua kiuchumi.
Naye rais wa shirikisho sanaa na ufundi Tanzania Adrian Nyangamale aliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuwakopesha wadau wa sanaa ambao hapo mwanzo walikuwa hawakubaliki kwenye mikopo kupitia Taasisi za kifedha.
Naye rais wa shirikisho la sanaa na maonesho Cynthia Henjewele alisisitiza wasanii kuitumia vyema mikopo watakayopewa ili iwainue kiuchumi na kuanza kuvhangia Pato la Taifa.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Hadija Kidevu alisema akifanikiwa kupokea mkopo kutoka Kwa Rais Samia atahakikisha anaboresha na kuendeleza Biashara zake za upambaji maharusi na kuimba taarabu ili kujikwamua kiuchumi.