Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, mzozo wa kisiasa unaoendelea Niger huenda ukaongeza ukosefu wa usalama wa chakula kwenye taifa hilo masikini, ukiomba kuondolewa kwa vikwazo na kufungwa kwa mipaka ili kuruhusu upelekaji wa misaada ya kibinadamu.
Ofisi ya masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA), imesema kwamba hata kabla ya rais wa taifa hilo aliyechaguliwa kidemokrasia Mohamed Bazoum kuondolewa madarakani kwa mapinduzi, tayari taifa hilo lilikuwa na zaidi ya watu milioni 3 ambao hawakuwa na usalama wa chakula.
Wengine milioni 7 ambao hali yao ilikuwa nafuu kidogo huenda wakafikia viwango vya ukosefu wa usalama wa chakula kabisa, iwapo hali itaendelea kama ilivyo, OCHA imeongeza, ikitaja uchambuzi uliofanywa na shirika la chakula duniani, WFP.
Niger inashuhudia hali ya wasiwasi baada ya mapinduzi ya kijeshi ya hivi karibuni.