Mgombea katika uchaguzi ujao wa urais nchini Ecuador ambaye alifanya kampeni dhidi ya ufisadi na magenge ya uhalifu ameuawa kwa kupigwa risasi kwenye mkutano wa kampeni.
Fernando Villavicencio, mjumbe wa bunge la kitaifa la nchi hiyo, alishambuliwa alipokuwa akiondoka kwenye hafla hiyo katika mji mkuu, Quito, siku ya Jumatano.
Yeye ni mmoja wa wagombea wachache wanaodai juu ya uhusiano kati ya uhalifu uliopangwa na maafisa wa serikali nchini Ecuador.
Genge la wahalifu liitwalo Los Lobos (The Wolves) limedai kuhusika.
Los Lobos ni genge la pili kwa ukubwa nchini Ecuador lenye wanachama 8,000, wengi wao wakiwa gerezani.
Genge hilo limehusika katika mapigano kadhaa ya hivi majuzi yaliyosababisha vifo vingi, ambapo wafungwa wengi wameuawa kikatili.
Kundi la watu waliojitenga na genge la Los Choneros, Los Lobos inaaminika kuwa na uhusiano na Jalisco New Generation Cartel (CJNG) yenye makao yake Mexico, ambayo inasafirisha cocaine.
Tuhuma za mauaji hayo ziliangukia kwa mara ya kwanza Los Choneros, ambayo ilikuwa imemtishia Bw Villavicencio wiki iliyopita, lakini Los Lobos ilidai kuhusika katika video ambayo washiriki wa genge waliovalia vazi walionyesha ishara za genge na kutikisa silaha zao.