Klabu za ligi kuu nchini Hispania zinatarajiwa kufanya mgomo mwishoni mwa wiki hii ambapo hakutakuwa na michezo yoyote kufuatia kushindwa kupatikana kwa makubaliano katika mkutano uliofanyika kati ya shirikisho la wachezaji , uongozi wa ligi pamoja na shirikisho la soka la Hispania .
Mgomo huu unakuja baada ya taarifa toka Serikalini ambayo iliarifu juu ya kuwepo kwa makubaliano mapya ya mikataba ya televisheni ambapo timu zote 20 zitaweza kufanya makubaliano ya mkataba wa haki za matangazo ya televisheni kwa umoja na sio tofauti na klabu kubwa za Real Madrid na Barcelona .
Umoja wa wachezaji unahisi kuwa bado matatizo yanayohusu malipo na haki zao hayajapewa kipaumbele na hivyo kwa kauli moja wamekubaliana kufanya mgomo ambao kimsingi utavuruga ratiba ya ligi ya Hispania .
Rais wa umoja wa wachezaji AFE Luis Rabes amethibitisha kuwa hakuna muafaka uliofikiwa na pande zote katika kikao kilichofanyika hii leo (jumanne) na kwa jinsi hali ilivyo hakutakuw ana michezo ya ligi ya Hispania wikiendi hii .
Hata hivyo bado kuna nafasi ya hali hii kubadilika kwani pande zote zinazohusika kwenye mazungumzo haya zitakutana katika mazungumzo mengine hapo kesho na endapo muafaka utafikiwa basi huenda michezo ya mzunguko wa 37 ikaendelea .
Hadi sasa Fc Barcelona ndio wanaongoza ligi na watajihakikishai kutwaa ubingwa endapo watashinda mchezo wao dhidi ya Atletico Madrid siku ya jumapili huku wakiwaacha mabingwa watetezi Atletico Madrid wakishindwa kutetea ubingwa wao .