Polisi Kilimanjaro inamshikilia mzee Mungai Molel (75) kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa miaka 11 wa shule ya msingi Okaseni na kumjeruhi vibaya katika sehemu za siri.
Kamanda wa Polisi mkoani humo Geofrey Kamwela amethibitisha kutokea kwa tukio hilo liliotokea Novemba 12, Kijiji cha Kitandu kata ya Uru Kusini ambapo mtuhumiwa huyo alimwita mtoto huyo nyumbani kwake na kumfanyia kitendo hicho cha kikatili.
“Alimwita nyumbani kwake na kumbaka na kumsababishia maumivu makali sehemu za siri na kusababisha mtoto huyo kulazwa katika Hospitali ya KCMC kwa matibabu kutokana na kuharibika vibaya sehemu za siri” — Kamwela.
Alisema mzee huyo alimbaka mtoto huyo hali iliyosababisha mtoto huyo kupiga kelele na kuokolewa na majirani wa mzee huyo na kutoa taarifa Polisi baada ya kumkuta mtoto huyo akivuja damu nyingi.
Mtuhumiwa huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi zaidi na atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.
MWANANCHI
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Mengwe Adinani Kingazi, amemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela Godfrey Kimaria (35) baada ya kukutwa na hatia ya kumjeruhi mtoto wa miaka minne kwa kumg’ata mgongoni akimtuhumu kumuibia paka.
Kesi hiyo ilivuta hisia za watu Wilayani Rombo Mkoani Kilimanjaro ambapo wananchi walifurika katika mahakama hiyo kusikiliza hukumu ya kesi hiyo.
Akitoa hukumu hiyo hakimu Kingazi alisema tarehe 29 Septemba mwaka huu katika Kijiji cha Msera juu, mshtakiwa alifanya kosa hilo kinyume cha kifungu cha sheria 214 cha sheria ya makosa ya jinai.
Hakimu huyo alisema mshtakiwa alifanya ukatili huo kwa mtoto Dilex Lyakurwa (09), ambapo mshtakiwa alimshambulia mtoto huyo kwa kile alichodai kuwa mtoto alienda kuchota maji nyumbani kwake, wakati akiwa anarudi kwenda nyumbani paka wa mshtakiwa alimfuata mtoto, baadaye paka huyo aligoma kurudi, ndipo mshtakiwa alimshambulia kwa madai kuwa amemuibia paka wake.
Mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka pamoja na vielelezo vya Polisi ikiwemo taarifa ya Daktari iliyoonyesha mtoto huyo aliumizwa kwa kuchomwa na kitu chenya ncha kali mgongoni.
Mshtakiwa anatumikia kifungo cha miaka mitatu jela na baada ya kumaliza adhabu atamlipa mlalamikaji shilingi laki mbili kama gharama za matibabu na fidia ya maumivu aliyoyapata.
NIPASHE
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mrisho Gambo, ameliagiza Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Lucas Mweri, kumchukulia hatua daktari anayedaiwa kumbusu mgonjwa wake wakati akimpa matibabu.
Gambo alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko ya tukio hilo na kueleza kuwa ni ukiukwaji wa maadili ya Udaktari na aibu kwa Wilaya.
Aliliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa mtaalam huyo na wengine wenye tabia kama hiyo.
Inadaiwa daktari Ally Naah anayefanya kazi Hospitali ya Wilaya ya Magunga, anadaiwa kumbusu mwanamke aliyekuwa akimpatia matibabu Hospitalini hapo.
Mashuhuda wanasema siku ya tukio mwanamke huyo aliongozana na mume wake kwa ajili ya kupata matibabu na baada ya kufika Daktari alimtaka aingie ndani kumfanyia uchunguzi, huku mume wake akiwa nje akimsubiria na baada ya kumsubiria kwa muda mrefu alipata hofu, ndipo alipochungulia dirishani na kumkuta daktari akimbusu mke wake.
“Yule bwana hakuamini alichokiona hakuvumilia alipiga kelele kuomba msaada.. kwa kweli jambo hili ni aibu na limetuondolea uaminifu” alisema mmoja wa shuhuda wa tukio hilo ambalo tayari Polisi wameanza kulifanyia uchunguzi.
Mganga mkuu wa wilaya ya Korogwe, Dk Olden Ngasa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema daktari huyo alitoroka baada ya tukio hilo.
HABARI LEO
Watoto watatu kutoka kijiji cha Barca huko Arber Wilayani Oyam Uganda, wanazungumza lugha isiyofahamika baada ya kufungiwa ndani ya nyumba yao kwa miaka saba, Lugha hiyo mpya imetajwa na watu wa jamii hiyo kuwa Leb-ad-am, ikimaanisha lugha ya ubongo.
Inadaiwa Baba wa Watoto hao aliwafungia ndani ili kuwalinda kutokana na hatari mbalimbali, watoto hao hawajaathirika kiakili bali hawawezi kuzungumza na watu wengine huku wakiamini kile baba yao anachowaambia.
Mama yao amesema watoto hao waliweza kuishi kwa kula mayai ya Chura yaliyochemshwa na majani, ambayo hula kila asubuhi na jioni na kutumia maji kutoka katika shimo lililochimbwa na baba yao.
Baba wa watoto hao alimzuia mama yao kuzungumza nao kwa kipindi chote, hatua hiyo iliwafanya kutojifunza lugha yao ya Kiluo wakati walipokuwa wadogo.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Mwanza limemfukuza kazi Askari wake Sajini WP Fatuma, baada ya kudhibitika kuwa alimkata vidole vinne mfanyakazi wake wa ndani Steven Magesa(18)
Kamanda wa Polisi Mwanza Valentine Mlowola, alisema baada ya kupokea taarifa za tukio la Askari huyo lililotokea Oktoba 20 mwaka huu , walichukua hatua za kiutawala na kuanza kufanya uchunguzi kufuatia tukio hilo, lililofanyika katika Kijiji cha Magange Mugumu Wilayani Sengerema Mkoani Mara ambapo ni nyumbani kwa kijana huyo, na walipata udhibitisho wa kutosha wa Askari huyo kuhusika na kosa hilo, hivyo kumfukuza kazi baada ya kumsikiliza katika Mahakama ya Jeshi.
“Baada ya uchunguzi tulibaini kuwapo kwa udanganyifu wa maelezo yaliyotolewa na WP Fatuma kuhusiana na tulkio hilo, hivyo kutokana na ushahidi uliowasilishwa katika Mahakama ya Jeshi, tulimtia hatiani na kuvuliwa nyadhifa zake zote ikiwa ni pamoja na kumfukuza kazi,
“Kwa sasa WP Fatuma amesafirishwa kwenda Mkoani Mara kwa ajili ya kushitakiwa Mahakamani kwa kosa la Jinai, hili ni fundisho kwa Askari wetu wengine wenye tabia kama hii na watu wengine ambao wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi na kufanya vitendo vya Jinai kwa kushindwa kufuata sheria”, alisema Mlowola.