MWANANCHI
Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam ameagiza Halmashauri ya Jiji kuziondoa haraka kampuni zote za udalali zinazokamata magari yanayovunja Sheria za maegesho baada ya kuongezeka malalamiko ya vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na kampuni hizo.
Baadhiya Kampuni ambazo zimetajwa ni Yono Auction Mart & Co Ltd, Tambaza Auction Mart & General Court of the Tribunal na Mwamkinga Auction Mart.
Baadhi ya kero zilizotajwa ni pamoja na kukamata magari yaliyopaki kwenye nyumba za watu, wamiliki wa magari kulazimishwa magari yao kuvutwa wakati yana uwezo wa kutembea yenyewe, kufukuzwa kwa magari kwa madai kwamba yameegeshwa vibaya, pamoja na kutozwa faini kubwa tofauti na kiwango kilichowekwa kisheria.
Sadiki amezishauri Halmashauri za Dar kuingia mkataba na Kampuni ya Ulinzi na Usalama ya Suma JKT kufanya shughuli hiyo kuliko utaratibu uliopo sasa.
MWANANCHI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia, John Mngondo amesema Nchi za Afrika bado zinakabiliwa na changamoto kubwa ya wakazi wengi kutokuwa na anuani za makazi ambapo sababu hiyo inatajwa kama moja ya sababu zinazopelekea kucheleweshwa kwa maendeleo.
Katibu Mkuu huyo ameyasema hayo katika Mkutano wa siku tatu uliowashirikisha wadau wa Posta ulioandaliwa na Umoja wa Posta Afrika (PAPU) pamoja na wadau wengine, huku akiongeza kuwa changamoto hiyo inachangiwa na miundombinu mibovu.
MTANZANIA
Umoja wa waendesha Bodaboda na Bajaj Dar es Salaam wamesema wanampa Rais Kikwete siku 14 kushughulikia maombi yao ya kuruhusiwa kusafirisha abiria katikati ya Jiji kinyume na hapo wataitisha maandamano ya amani kushinikiza ombi lao kutekelezwa.
Mwenyekiti wa Chama hicho Said Chenja amesema hawaridhishwi na namna ambayo watendaji wa chini wa Rais wanavyoshughulikia suala hilo.
Mwenyekiti huyo amesema suala la utoaji wa vibali maalum limekuwa likifanywa kwa upendeleo mkubwa huku vibali hivyo vikiwa na mapungufu ya kutokuwa na maelekezo ya maeneo ambayo wale waliopewa vibali hivyo wanaruhusiwa kuingia na ambako hawaruhusiwi.
JAMBO LEO
Kiwanda cha kuzalisha Sukari cha Kilombero kiko hatarini kufungwa kutokana na kukosekana kwa soko la Sukari inayozalishwa kiwandani hapo ambapo jumla ya ajira 75,000 na zaidi ya wakulima 15,000 wanaolima zao hilo pia kujikuta wakipoteza vyanzo vya mapato.
Wakulima na wafanyakazi hao wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuinusuru hali hiyo huku kwani maisha yao yanategemea kiwanda hicho kwa asilimia kubwa.
Changamoto ya uingizwaji wa Sukari kutoka nje bila kutoza ushuru imeathiri sehemu kubwa ya soko la bidhaa hiyo ndani ya nchi.
NIPASHE
Mama mmoja mjamzito, Grace Frederick na mtoto wake Braiton Said mwenye umri wa miezi 11 walikamatwa na Polisi Chato, December 07 mwaka huu baada ya kudaiwa kumfungia wifi yake, Mwanvua Said ambaye inasemekana alitaka kuhamisha vitu bila taarifa ya mume wake.
Grace aliwekwa ndani na mtoto wake ambaye anasema wakati wa usiku alilia sana kutokana na kushikwa na njaa.
Hii ni kinyume na ambavyo inatakiwa kufanyika kwani Serikali na Mashirika mbalimbali wamekuwa wakiendesha kampeni za kupunguza vifo vya Wanawake wajawazito na watoto chini ya mwaka mmoja.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chato, Alex Musama alisema kuwa hajapata taarifa zozote kuhusu madai hayo.
Unahitaji kupata story zote kali zinazonifikia? Ni rahisi sana mtu wangu.. Niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook