MWANANCHI
Wakati Eliakim Maswi aliporejeshwa kuwa katibu tawala wa mkoa akitokea nafasi ya kaimu naibu kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Ikulu ilisema uamuzi huo ulitokana na kumaliza kazi maalumu, lakini wanasiasa wamedai kuwa, amehamishwa kupunguza hasira za Bunge.
Maswi alikuwa katibu mkuu wa Wizara ya Nishati, lakini aliondolewa wakati wa sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow kwa madai kuwa hakuwajibika ipasavyo kuokoa fedha za Serikali, lakini miezi michache baadaye Ikulu ilitoa taarifa kuwa mrasimu huyo ameonekana hakukiuka maadili katika sakata hilo baada ya kuchunguzwa na Baraza la Maadili ya Viongozi.
Kauli hiyo ilifuatiwa na uamuzi wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kumteua kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara na baadaye Rais John Magufuli kumteua kuwa kaimu naibu kamishna wa TRA, kabla ya kumrejesha kwenye nafasi yake mkoani Manyara mapema wiki hii, akisema amemaliza kazi aliyotumwa.
Lakini wabunge na wasomi waliohojiwa na Mwananchi wamesema Rais amechukua hatua hiyo baada ya kukosolewa na wanasiasa na wadau mbalimbali wanaodai kuwa Maswi hakustahili kupewa wadhifa huo baada ya sakata hilo la Escrow.
“Amefanya hivyo kuepuka mjadala utakaojitokeza kwenye Bunge la Kumi na Moja kuhusu escrow,” alisema mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye aliibua sakata hilo bungeni mwaka 2014.
“Kuna hatari mada ya ufisadi ikaibuka kwa njia nyingine kwenye Bunge kwa kuanza kuwazungumzia hawa wahusika ambao wamerudishwa kwa namna ya pekee na kupewa nafasi nyeti,” alisema Kafulila, ambaye amefungua kesi akitaka Mahakama itengue matokeo ya ubunge na kumtangaza kuwa mshindi.
Alisema kwa nafasi aliyokuwa nayo Maswi wakati wa sakata la Escrow, hana pa kukwepea, akidai kuwa anaweza kuhusika kwa uzembe au kwa kukusudia.
“(Rais) Amemuondoa kupunguza Serikali kupingwa na wabunge kutokana na kuwabeba waliohusika na kashfa mbalimbali ikiwamo Escrow. Lakini bado kuna watu amewaacha kama (Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter) Muhongo na (Waziri wa Katiba) Dk Harrison Mwakyembe, ”alisema Kafulila na kuongeza.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyowasilisha ripoti ya sakata hilo bungeni, alisema Rais hakuwa na taarifa sahihi wakati anamteua Maswi.
Alisema hali kama hiyo ilitokea pia kwenye uteuzi wa Profesa Makame Mbarawa ambaye kwanza alitangazwa kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji na ndani ya siku chache akahamishiwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
“Hii inaonyesha hakuwa makini wakati anafanya uteuzi,” alisema Zitto. “Hatutegemei kuona uteuzi wa kubadilikabadilika.
Awachunguze kwa makini anaowateua na nafasi anazowapa ili kukwepa kuonekana kuwa hakuwa makini kama inavyoonekana sasa.” Profesa Damian Gabagambi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua) aliungana na Kafulila kwamba Rais amechukua hatua hiyo baada ya kuona kasi anayoitaka, itaingia doa hasa baada ya watu kulalamikia uteuzi wa Muhongo na Maswi. “Inawezekana wakati anamteua hakuwa akifahamu vitu vingi kumhusu (Maswi), lakini baada ya uteuzi maneno ya wadau, wasomi na watu mbalimbali yakamshtua na kufuatilia kwa umakini,” alisema.
Profesa Gabagambi alisema uteuzi wa viongozi siyo jambo dogo hasa unapotaka kuleta mabadiliko na mtazamo tofauti na uliokuwapo hapo awali.
“Unaweza kuwaona viongozi wachapakazi ambao ungeweza kuwateua, lakini kwa bahati mbaya wanatoka mkoa mmoja, hivyo ukiwateua italeta maneno.
Hapo ndipo panapoleta tabu kidogo,” alisema Gabagambi. Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco), alisema lengo la Rais Magufuli ni kujenga Serikali yenye heshima, anatamani asisikie kashfa ya aina yoyote ya ufisadi, lakini kuna baadhi ya watu inaonekana aliwateua kabla ya kufahamu kuwa wanahusika kwa namna moja aunyingine kwa kashfa hizo.
Alisema rais ana washauri ambao inawezekana walimpelekea taarifa kuhusu watu aliowateua, kazipima na kuona anaweza kuleta shida kuendelea kuwa nao hasa katika sehemu nyeti. “Siyo kwamba Rais hasikii watu, wadau, historia ya anaofanya nao kazi inasema nini, anasikia na hilo limeonekana katika uamuzi alioufanya kwa Maswi.
Ametafakari, amepima na kuona anatakiwa kufanya mabadiliko kama anataka kweli mambo yaende kama anavyotaka,” alisema Profesa Mpangala.
MWANANCHI
Siku moja baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kusema akionana na waliokuwa wanachama wa CCM na kuhamia upinzani anajisikia kichefuchefu, waliokuwa makada wa chama hicho wamemshukia kwa kauli yake hiyo.
Membe alitoa kauli hiyo hivi karibuni katika mahojiano maalumu na gazeti hili alipotakiwa kuwazungumzia makada wa chama hicho waliohama na kusisitiza kuwa wasipokewe endapo watataka kurudi.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye ambaye alitimkia Chadema, alisema kama angesikia maneno hayo kwa mtu mwingine asingeshangaa, lakini siyo kwa Membe.
Mbunge huyo wa zamani wa Arumeru – Magharibi, alisema Membe anapata masilahi yake kwa kutambulika kama waziri mstaafu na wakati anaapa kuwa katika nafasi hiyo alitumia Katiba ambayo hivi sasa kwa kupinga yaliyomo ikiwamo uhuru wa mtu kujiunga na chama chochote cha siasa, anakosea.
Medeye alisema kwa kauli hiyo, Membe hana haki ya kugombea nafasi yoyote ya siasa kwa sababu haamini katika vyama vingi wakati Taifa linaendeshwa kwa Katiba inayokubali suala hilo.
Alisema hata kauli ya Membe ya kutounga mkono uchaguzi kurudiwa Zanzibar akitaka kufanyiwa kazi kasoro chache ni ya kinafiki kwa sababu ameonyesha kutopenda upinzani. “Hana msimamo hazungumzi vitu kutoka moyoni, kama kweli anakubali vyama vingi na ana uchungu na kinachoendelea Zanzibar, kwa kuwa bado ni mjumbe wa Nec (Halmashauri Kuu ya CCM), angemuomba mwenyekiti wake aitishe mkutano mkuu lijadiliwe hilo na atoe anachokiamini, hakufanya hivyo kwa sababu hakubali vyama vingi, hataki mabadiliko katika siasa anayoitumikia, ” alisema Medeye.
Aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru alisema hawezi kujibizana na watu kwani anajua anachofanya. Alisema anayo mawazo huru na akitaka kuzungumza jambo lolote atafanya hivyo kwa utashi wake na siyo kujibizana na watu waliozungumza kwa utashi wao.
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita alisema anamheshimu Membe kwa sababu amefanya naye kazi katika chama hicho tawala na kumshauri siku nyingine anapozungumza mambo kama hayo asiegemee upande mmoja.
Alisema licha ya kuwa hayo ni mawazo yake na kila mtu ana uhuru wa kuwaza na kusema anachotaka, alipaswa apime anazungumza nini na kwa manufaa ya nani. Guninita alisema Katiba ya nchi inamruhusu mtu kuhama chama hata mara 10 alimradi huko anakokwenda atapata vitu muhimu ikiwamo malengo yake binafsi, ya chama husika na mafanikio ya Taifa.
Alisema haikuandikwa ni lazima abaki sehemu anayoamini hana malengo nayo, au asihame kutoka chama kimoja ama kingine.
MWANANCHI
Siku moja baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) kuitangaza Machi 20 kuwa siku ya marudio ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, mgombea urais, Maalim Seif Sharif Hamad na Edward Lowassa leo wanakutana na wabunge wote kutoka vyama vinavyounda Ukawa kutoa “tamko zito” litakalotoa mwelekeo wa hali halisi ya kisiasa visiwani humo.
CUF, ambayo inapinga kurudiwa huko kwa uchaguzi, nayo imepanga kufanya vikao vyake vya juu mapema wiki ijayo kuweka msimamo wake kuhusu tangazo hilo.
Wakati hayo yakiendelea, mabomu ya machozi jana yalilipuliwa kwenye maeneo tofauti ya Zanzibar wakati askari wa Jeshi la Polisi wakitawanya watu waliokuwa wamekaa kwenye vikundi, kwa kuhofia kuwa wanaweza kutumia mwanya huo kufanya vurugu.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha alitangaza juzi kuwa marudio ya uchaguzi hayatatanguliwa na kampeni za wagombea wa nafasi za urais, uwakilishi na udiwani na wala hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya wagombea.
Bado vyama vya upinzani havijatoa tamko kuhusu uamuzi huo wa ZEC, lakini viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, CUF, NLD na NCCR Mageuzi wanatarajiwa kuhudhuria kikao hicho kitakachofanyika kwenye Ukumbi wa African Dream.
Habari zilizolifikia gazeti zinaeleza kuwa awali katika kikao hicho Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulipanga kujadili mkwamo wa kisiasa na jinsi ya kupata suluhu, lakini baada ya ZEC kutangazaa kurudiwa kwa uchaguzi huo, ajenda imebadilika na sasa umoja huo utatoa msimamo wake wa mwisho kuhusu Zanzibar.
Msemaji wa Lowassa, Aboubakar Liongo na Ismail Jussa walithibitisha viongozi hao kutua Dodoma jana jioni tayari kwa kikao hicho ambacho kitaanza asubuhi.
Habari zaidi zinaeleza kuwa awali, Maalim Seif na Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu na ambaye mwaka jana aligombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema, watakutana na viongozi wakuu wa Ukawa na baadaye na wabunge wote na kisha kutoa maazimio.
“Ni maazimio ambayo yanalenga kueleza ukweli kuhusu kinachotaka kufanyika Zanzibar. Yatakuwa maazimio mazito,” alisema mpashaji habari wetu.
Januari 20, wabunge wa Ukawa walifanya kikao cha ndani kwenye ukumbi wa Pius Msekwa uliopo viwanja vya Bunge kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar na kutangaziwa kuwa wataelezwa msimamo wa umoja huo leo.
“Watapewa mrejesho wa kikao cha mwisho kati ya Maalim Seif na (Rais wa Zanzibar) Dk Ali Mohamed Shein. (Mwenyekiti wa Chadema, Freeman) Mbowe na mwanasheria wa Chadema (Tundu Lissu) nao wataeleza masuala mbalimbali kuhusu Zanzibar,” alisema mtoaji habari huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Mwenyekiti wa NCCRMageuzi, James Mbatia alisema licha ya kuwapo kwa mazungumzo hayo, msimamo wa Ukawa na CUF wa kupinga uchaguzi huo kurudiwa, upo palepale.
“Kesho (leo) tunazungumza kuhusu Zanzibar. Pamoja na mambo mengine tutatafakari hali ya kisiasa visiwani Zanzibar na nchi kwa ujumla na baada ya hapo tutatoa maazimio yetu,” alisema Mbatia.
Alisema lengo la kikao hicho ni kuelezana kwa kina lilipo tatizo, kupewa taarifa na takwimu sahihi. “Hatuko tayari kurudiwa kwa uchaguzi Zanzibar, Watanzania lazima wakumbuke kuwa ukitenda haki, amani ndipo hupatikana,” alisema. Alisema kutokana na kufutwa kwa uchaguzi huo, Tanzania imetengwa pamoja na kunyimwa fedha za maendeleo kutoka mataifa makubwa. “Ole wao wanaofanya mambo haya.
Yakisababisha umwagaji damu yatawagharimu na wapo watakaokamatwa na kufikishwa Mahakama ya Kimataifa kwa kusababisha mauaji,” alisema Mbatia. “Suala la Zanzibar hatukubaliani nalo kwa sababu ukishawekwa utaratibu, halafu ukauvuruga ni fujo.
Na duniani kote dola na taasisi huundwa kwa njia ya maridhiano,” alisema. “Mwaka 1995 na 2000 mauaji yalitokea Zanzibar lakini mwaka 2010 hayakutokea kwa sababu ya maridhiano ya CCM na CUF. “Leo hii Zanzibar wanarudi kulekule kwa kuwa CCM wasiposhinda inakuwa nongwa.
Wanataka wao ndiyo washinde tu na wanadhani wao ndiyo wenye fikra na haki tu. Kama ni hivyo kwa nini mfumo wa demokrasia uwepo?” Wakati mkutano huo ukiandaliwa, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Umma wa CUF, Jussa, ambaye amelielezea tamko la Jecha kuwa halizingatii Katiba wala sheria. Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Jussa amelielezea tamko hilo kuwa “la kihuni lisilozingatia Katiba wala sheria” na kwamba vikao vya juu vya chama hicho vitafanyika mapema wiki ijayo kufanya uamuzi.
“Kamati ya Utendaji ya Taifa itakutana tarehe 27 Januari, 2016 na kufuatiwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa litakalokutana Alhamisi, tarehe 28 Januari, 2016,” inaeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Jussa akiongeza kuwa vikao hivyo vitafanyika kwenye ofisi za makao makuu ya CUF zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo inawataka wananchi ambao kinasema “waliikataa CCM kwa kishindo Oktoba 25”, kuendelea kutunza amani na kuwa watulivu “katika kipindi hiki kigumu na kusubiri maamuzi ya chama chao wanachokiamini”.
Akitangaza tarehe ya kurudia uchaguzi huo juzi kupitia kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ambako pia Januari 28, 2015 alitangaza kuufuta, Jussa alisema kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi.
Alisema uchaguzi huo utarudiwa ndani ya siku 90. Juhudi za kutafuta suluhisho la kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo zilizomshirikisha Dk Shein na Maalim Seif zimegonga mwamba baada ya kufanya vikao tisa bila kuafikiana. Tayari Maalim Seif ameshajitoa kwenye mazungumzo hayo yaliyohusisha vikao tisa
MWANANCHI
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa ufafanuzi kuhusu mavazi ya kijeshi ambayo Rais John Magufuli alivaa juzi wakati akienda Chuo cha Maofisa wa Jeshi cha Monduli (TMA) mkoani Arusha.
Dk Magufuli alivaa vazi hilo lenye mabaka ya rangi ya mchanganyiko ya kijani, kahawia nyeusi na nzito, lakini haikuwa na alama za cheo mabegani wala kifuani, jambo lililosababisha mjadala mkubwa hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Kilichokuwa kikihojiwa zaidi ni sababu za kutoa alama hizo wakati akiwa kwenye taasisi ambayo utambuzi wa cheo hutegemea nishani hizo. Msemaji wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema jana kuwa hakukuwa na tatizo lolote kwa Rais Magufuli kuvalia mavazi hayo bila alama za vyeo na wala kuyatumia wakati akihutubia wananchi.
Kanali Lubinga alisema Sheria ya Jeshi ya Mwaka 1966 (National Defence Act) inamhalalisha Rais aliyepo madarakani kuvalia mavazi hayo kwa kuwa ni Amiri Jeshi Mkuu.
Kuhusu magwanda hayo kutoonyesha vyeo, Lubinga alisema tofauti na wanajeshi wengine, sare za Amiri Jeshi Mkuu hazina vyeo wala alama yoyote mabegani.
Juzi, kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii watu walituma picha inayomuonyesha Rais Magufuli katika mavazi hayo sambamba na picha ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye gwanda lake lilikuwa na nyota nne.
Pia, picha hizo ziliwaonyesha viongozi wa zamani, Mwalimu Julius Nyerere, Samora Machel wa Msumbiji na Kenneth Kaunda wa Zambia wakiwa wamevalia magwanda ya kijeshi, lakini ambayo hutumiwa kwenye shughuli za kawaida.
Picha nyingine zilimuonyesha Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Barack Obama (Marekani) na Paul Kagame wa Rwanda wakiwa kwenye magwanda hayo.
Kuhusu kuvalia mavazi hayo wakati akihutubia wananchi uraiani, Lubinga alisema alilazimika kuhutubia wakati akiwa njiani kuelekea chuo hicho cha kijeshi cha Monduli.
“Watanzania waelewe kwamba kitendo cha Rais kuvalia mavazi ya kijeshi si cha ajabu kwa sababu alikuwa kwenye shughuli za kijeshi na nafasi yake ya Amiri Jeshi Mkuu inampa haki hiyo,” alisema.
Alisema Rais alikuwa anakwenda kwenye majukumu ya kijeshi, lakini kutokana na watu kumtaka kwa kumfungia barabara, alilazimika kusimama na kuzungumza nao kukata kiu.
“Baada ya msafara wake kusimamishwa wakati akielekea Chuo cha Maofisa wa Jeshi, haikuwezekana kurudi ili abadilishe mavazi ndipo arudi kuzungumza nao, ikalazimika azungumze na wananchi wake akiwa katika mavazi hayo,” alisema Kanali Lubinga
HABARILEO
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhan Kailima, amesema wabunge wa Viti Maalumu wanaruhusiwa kuwa madiwani katika maeneo wanakotoka.
Alitoa ufafanuzi huo jana, alipozungumza na gazeti hili kuhusu hatua ya vyama vya siasa, ikiwemo CCM kuongeza idadi ya madiwani wake kutoka kundi la wabunge wa viti maalumu, katika chaguzi za mameya hasa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kailima, Sheria ya Serikali za Mitaa inatambua kuwa kila mbunge ni diwani katika eneo anakotoka, hivyo wabunge wa viti maalumu, ni madiwani katika maeneo wanakoishi.
Kwa kuzingatia sheria hiyo, wabunge wa viti maalumu wanapoomba nafasi hiyo ndani ya vyama na kuteuliwa, Kailima alisema, wanatakiwa kujaza fomu namba 8D ya NEC inayoelezea maeneo wanayoishi, ambayo ndiyo inayotumika kuwapa uhalali wa kuwa madiwani katika maeneo hayo.
Maombi ya CCM, Chadema Kailima alisema mwishoni mwa wiki, vyama vya CCM na Chadema waliandikia barua kwenda NEC kuomba uthibitisho wa makazi ya wabunge wake wa viti maalumu, ili utumike kuwaidhinisha kuwa madiwani katika halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema CCM walikwenda na barua ikiwa na orodha ya madiwani inaotaka wathibitishwe ukazi wao na nakala ya fomu namba 8D, ambayo mbunge husika wa viti maalumu alijaza kabla ya kuteuliwa, inayoonesha anuani ya eneo analoishi.
Hivyo CCM kwa mujibu wa Kailima, walithibitisha makazi na anuani ya wabunge wanaoishi Kinondoni, wakajiridhisha kisha wakachukua fomu yenye majina ya wabunge wote wa viti maalumu na kuweka alama ya tiki katika majina ya wabunge wanaostahili kuwa madiwani katika Halmashauri ya Kinondoni.
Alisema baadae Chadema walikwenda NEC na barua, lakini bila nakala ya fomu namba 8D, hata hivyo kwa kutumia fomu hizo zilizopo NEC, wakathibitisha wabunge wa viti maalumu wa chama hicho waliokuwa wakazi na wasio wakazi wa Kinondoni, mbele ya Mwenyekiti wao Freeman Mbowe na ofisa wao mmoja.
Kailima alisema kabla ya Mbowe kuondoka, aliomba kuthibitisha pia wabunge wa viti maalumu ambao ni wakazi wa Ilala bila kuwa na barua, ambapo aliruhusiwa kuthibitisha.
Alisisitiza kuwa kazi hiyo ya kuthibitisha ukaazi wa wabunge wa viti maalumu, ili kutambua wanakoweza kuwa madiwani, inafanywa na NEC kwa kuwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), hawana uwezo kutoa uthibitisho huo.
Hivi karibuni, wakati wa uchaguzi wa Meya wa Kinondoni, vyama vya upinzani vililalamika kuburuzwa katika uchaguzi huo, kwa madai kuwa CCM ilitaka kuongeza madiwani wa Viti Maalumu tisa, kutoka kundi la wabunge wa viti maalumu.
Vyama hivyo vilidai kuwa, hatua ya wabunge hao wa viti maalumu kuwa madiwani wa viti maalumu Kinondoni, ni uchakachuaji wa wazi wa kura za kumpata Meya wa manispaa hiyo.
HABARILEO
Bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kutoka Marekani kwa ajili ya kutolewa msaada kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime zimeteketezwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kwa sababu ya kutofaa kwa matumizi ya binadamu.
Shirika hilo pia limeteketeza nepi zinazotumika mara moja na kutupwa, ziitwazo Smart Baby, kwa kuwa hazikidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa na kwa sababu zimekwisha muda wa matumizi.
Akizungumza baada ya bidhaa hizo kuteketezwa katika dampo la Pugu Kinyamwezi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam juzi, msemaji wa TBS, Roida Andusamile alisema bidhaa zote zina thamani ya Sh milioni 20.
Kwa mujibu wa Andusamile, wakati bidhaa zilizoingizwa kwa ajili ya Halmashauri ya Tarime zililetwa zitolewe msaada kwa wahitaji kwenye eneo hilo, na nepi ziliingizwa nchini ili ziuzwe.
Aliitaja kampuni iliyoingiza nepi hizo kutoka China kuwa ni Chaoming & Xlambin Chen, iliyolenga kuzisambaza katika soko la ndani na kwa faida.
Andusamile alisema, “kwa kawaida bidhaa mbalimbali zinapoingizwa nchini kutoka nje kwa ajili ya biashara, kupitia katika mipaka yetu, bandari na viwanja vyetu vya ndege hukaguliwa na maofisa wa udhibiti ubora kutoka TBS, ili kujiridhisha endapo zinafaa kwa matumizi au la”.
Alisema baada ya kukagua mizigo hiyo katika bandari ya Dar es Salaam na kupima sampuli kwenye maabara husika za shirika hilo, yalibainika mapungufu kadhaa, ikiwemo kwisha kwa muda wa matumizi.
Ofisa Udhibiti Ubora wa TBS, Salome Emmanuel alieleza kuwa, mbali ya muda wa matumizi ya nepi hizo kwisha, vipimo vya sampuli za bidhaa hiyo vilionesha kuwa hazifai kutumiwa kuvalishwa watoto, kwa sababu zina madhara kwa afya zao.
Bidhaa za msaada ambazo watu wa Marekani wanaelezwa kuchanga ili kusaidia wahitaji Tarime, ambazo hata hivyo ziliteketezwa ni losheni za watoto, sabuni za maji kwa ajili ya kunawa mikono, dawa za meno aina ya Colgate na Crest.
Nyingine ni dawa za kusukutua mdomo ili usinuke, sabuni za kuoshea nywele pamoja na sabuni za maji za kuogea. Ilielezwa kuwa bidhaa hizo zilibainika mwishoni mwa mwaka jana, na kwamba zilizoingizwa kibiashara ziliteketezwa kwa gharama za kampuni iliyoagiza huku za msaada zikiteketezwa na TBS.
HABARILEO
Serikali imeombwa kuwaruhusu wafanyabiashara wa nafaka waliopewa vibali vya kufuata mahindi katika Maghala ya Hifadhi za Chakula ya Taifa (NRFA) kuwauzia mahindi na siyo unga wa sembe tu katika wakati wa kipindi hiki cha kukabiliana na upungufu wa chakula katika maeneo yao.
Ombi hilo lilitolewa juzi na baadhi ya wananchi katika kijiji cha Zanzui wilayani humo wakati wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho kujionea jinsi wanavyokabiliwa na upungufu wa chakula.
Walisema kuwa kitendo cha serikali kuwaagiza wafanyabiashara hao kuyasaga mahindi hayo na kuwauzia unga kwa bei elekezi ya shilingi 900 kwa kilo badala ya mahindi, kunawafanya waendelee kukabiliwa na upungufu wa chakula kwani wengi wao wanapenda kununua mahindi badala ya unga.
“Serikali yetu imefanya vizuri kuwapatia vibali na kuwaruhusu hawa wafanyabiashara kununua mahindi hayo kwa bei nafuu huko Sumbawanga hadi kuyaleta hapa wilayani kwetu Maswa, lakini pia tunaomba iwaruhusu ili waweze kutuuzia mahindi kwa bei itakayopangwa na serikali na siyo unga,”alisema Yunge Lutonja.
Walisema kuwa wakinunua mahindi yatawawezesha kumudu njaa inayowakabili, ikiwa ni pamoja na hata kupika makande badala ya uji na unga tu huku wengine wakilalamikia kuwa katika maeneo yao ya vijijini huwa hawatumii unga wa sembe isipokuwa unga wa dona.
Mfanyabiashara wa nafaka Thomas Ndaki ambaye pia ni mmiliki wa Kiwanda cha Kusaga na kukoboa nafaka cha Ndaki Posho Mill kilichoko katika kijiji cha Zanzui wilayani humo alisema kuwa licha ya changamoto za kusafirisha mahindi hayo kutoka katika maghala ya Taifa yaliyoko katika mikoa ya Katavi na Rukwa lakini wanakabiliwa na malalamiko ya wananchi kutaka wauziwe mahindi badala ya unga.
NIPASHE
Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), kimesema gharama ya kumsomesha mwanafunzi wa urubani na wahandisi wa ndege ni Sh.milioni 10 hivyo kimeiomba serikali kupitia Bodi ya Mikopo iweze kuwasaidia wanafunzi wanaochukua kozi hizo.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji Mhandisi Dk. Zacharia Mganilwa, wakati wa uzinduzi wa ‘Banda’ la ndege litakalotumika katika mafunzo ya wahandisi wa ndege na marubani.
Alisema gharama hizo ni kubwa kulinganisha na kozi nyingine zinazotolewa hapa nchini.
Alisema Bodi ya Mikopo imekuwa ikitoa mkopo usiozidi Sh. milioni 1.5 kwa mwanafunzi ambaye ada yake ni Sh. milioni kumi.
Mganilwa alisema gharama kubwa zimekuwa zikibebwa na mzazi, zaidi ya Sh. milioni tisa.
“Sh. milioni tisa ambazo anatakiwa alipe mzazi imekuwa kwa kiasi fulani changamoto kwao hivyo ninaomba bodi ya mikopo iweze kuliangalia suala hili, waongezewa hata kidogo,” alisema.
Mganilwa aliongezea kuwa kwa hivi sasa marubani wengi na wahandisi wa ndege wamezeeka na wengine kustaafu hivyo kuiacha sekta ya anga kuwa na Watanzania wachache na wengi wageni.
“Mipango na mikakati yetu mikubwa ni kuona tunazalisha watanzania wengi kabisa katika eneo hili la mafundi wa ndege na marubani, hatutaki kuachia wageni tu waweze kuajiliwa katika sekta hii ya anga nchini,” alisema.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Faustine Kamuzola, alisema serikali itatoa kila aina ya msaada kwa NIT ili kiweze kuzalisha marubani na wahandisi wa ndege wa kutosha katika kukuza sekta ya anga nchini.
Profesa Kamuzola alisema serikali itashirikiana na Sekta binafsi katika kukisaidia chuo hicho kiweze kufikia malengo yake ya uzalishaji wa rasilimali watu katika sekta ya usafirishaji.
“Tumesikia kutoka kwa mkuu wa chuo hiki kuwa ada ya kumfundisha rubani wa ndege ama mhandisi ni Sh. milioni kumi, lakini tukimpeleka mwanafunzi nje ya nchi tutapaswa kulipa ada ya zaidi ya Sh. milioni 100, sasa serikali imewasikia,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa kutoa mafunzo haya kwa gharama ya bei nafuu kabisa, ana imani kwamba Watanzania wengi wenye nia ya kusomea urubani na uhandisi wa ndege watajiunga na chuo hicho.
NIPASHE
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeshauriwa kuondoa kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio Machi 20 mwaka huu.
Ushauri huo umetolewa kwa nyakati tofauti na baadhi ya wagombea wa Urais wa Zanzibar, wanasheria na wananchi walipokuwa wakizungumza na Nipashe Mjini Zanzibar baada ya tume kutangaza rasimi kufanyika kwa uchaguzi huo Machi 20 juzi.
Mgombea wa urais wa Chama cha AFP, Soud Said Soud alisema kuwa ili uchaguzi uwe huru na wa haki lazima kasoro za kiutendaji zilizojitokeza na kusababisha matokeo ya uchaguzi kufutwa zifanyiwe kazi ili kuepusha kujirudia kwa kasoro ikiwemo kuongezeka kura katika masanduku kinyume na idadi ya watu waliosajiliwa kwenye daftari la wapiga kura katika vituo vya uchaguzi.
Alisema hatua hiyo ndiyo njia pekee itakayosadia kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki na kumaliza tatizo la uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Soud alisema ni lazima kwanza wananchi wote wenye sifa wapate nafasi ya kuhakikisha wanashiriki kupiga kura bila ya kuwepo vikwazo na mazingira ya vitisho.
“Tume ya uchaguzi lazima wasimamie na kuondoa kasoro zilizojitokeza katika kuchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana, kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio Zanzibar,” alisema Soud.
“Vitendo vya udaganyifu na mizengwe havikubaliki katika utaratibu wa kupata viongozi waliochaguliwa kidemokrasia na wananchi.”
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed, alisema uchaguzi uliofutwa ulitawaliwa na vitendo vya udaganyifu katika vituo vya wapiga kura jambo ambalo linahitaji kuangaliwa na ZEC kabla ya kufanyika uchaguzi mpya.
Hata hivyo, alisema kuwa mfumo mzima wa muundo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kikatiba unahitaji kuangaliwa upya kwa kufanyiwa marekebisho ya kikatiba baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu.
Alieleza kuwa marekebisho ya Katiba yaliyofanyika na kuingiza wajumbe wa tume wanaotokana na vyama vya siasa, kumeongeza matatizo mkubwa na kukwamisha utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo.
Alisema tatizo la wajumbe wa ZEC kutawaliwa na utashi wa vyama katika utekelezaji wa majukumu yao kumechagia kwa kiasi kikubwa kujitokeza kwa matatizo na kulazimika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana kurudiwa Visiwani humo.
Aidha alisema sheria ya kuzuia maamuzi ya Tume ya Uchaguzi kuhojiwa Mahakamani imepitwa na wakati kwa sababu inawanyima wapiga kura uhuru wa Kikatiba wa kutumia mahakama, sheria zinapovunjwa na tume hiyo.
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) Omar Said Shaban alisema kurudiwa kwa uchaguzi Zanzibar sio ufumbuzi wa kumaliza mgogoro wa mkwamo wa uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Alisema njia pekee ya kumaliza mgogoro wa uchaguzi ni kurudi katika hoja ya msingi ya kufutwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu; kuangalia kama uchaguzi huo ulikidhi matakwa ya kisheria na Katiba kabla ya kufutwa matokeo na Mwenyekiti Jecha Salim Jecha Oktoba 28 mwaka jana.
Waangalizi wa kimataifa kutoka ndani ya Afrika na Ulaya walitangaza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 ulikuwa huru na wa haki kabla ya kufutwa siku chache baadaye na mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha.
“Kabla ya Mwenyekiti kutangaza tarehe ya uchaguzi alitakiwa kusema kifungu gani cha Katiba na sheria kimempa uwezo wa kufuta matokeo na kuitisha uchaguzi wa marudio,”alisema Shaban ambaye pia Wakili wa Mahakama kuu ya Zanzibar.
NIPASHE
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Frederick Shoo, amesema kasi ya Rais John Magufuli, ya kutumbua majipu inaridhisha na amemtaka akaze kamba kwani watanzania wako nyuma yake.
Aidha, Askofu Shoo amewasihi viongozi wenzake wa dini na madhehebu tofauti kuungana kumuombea Rais Magufuli ili kumnusuru na jambo baya kwasababu kazi anayofanya ni ngumu na inahitaji maombi.
Aliyasema hayo jana wakati akifanya mahojiano maalumu na gazeti hili kuhusu siku 80 za Rais Magufuli Ikulu.
Kwa tathmini ya Askofu Shoo, Magufuli ameonyesha uongozi mzuri na ushupavu, na ni kiongozi anayepaswa kuigwa na marais wengine duniani.
Alisema anafurahishwa na kasi ya utendaji kazi ya Rais kwasababu ndani ya muda mfupi ameonyesha umahiri kwa kuokoa mabilioni ya fedha zilizokuwa zikitafunwa na “wezi”.
Askofu Shoo alisema kazi ya Rais Magufuli inatia moyo kwa taifa na kanisa kwa ujumla, hivyo alimuasa aendelee na kasi hiyo kuibua ufisadi ambao ulikuwa ukisababisha kupotea kwa mabilioni.
Alisema wakati wa uongozi wa Hayati Mwalimu Julias Nyerere, uchumi ulikuwa imara na nchi ilikuwa ikijiendesha kwa rasilimali zilizoko, lakini baada ya kupita utawala wake mambo yamekuwa tofauti.
Alisema haijawahi kutokea katika historia ya nchi kwa kiongozi mkakamavu kama Magufuli kujitoa kwa maslahi ya taifa kwa kufichua wezi na kuwafukuza kazi kwani kwenye serikali zilizopita hawakuguswa.
“Labda niseme tu inawezekana Mungu amemwonyesha njia mtumishi wake Magufuli, kwa makusudi ili afichue mambo ambayo yakiboreshwa na kusimamiwa yataweza kuibadilisha nchi na kuwa miongoni mwa nchi za kuigwa kupitia ukuaji wa uchumi,” alisema Askofu Shoo.
Alisema anatarajia kutoa tamko lake mwanzoni mwa wiki ijayo kuhusu utendaji kazi wa Magufuli katika hatua za mwanzo za utawala wake, na kuwasihi viongozi wa dini mbalimbali kuungana katika maombi ili kumnusuru na jambo baya dhidi yake.
Alipoingia tu madarakani, Magufuli alisababisha mtikisiko mkubwa ndani ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kubaini mianya ya ukwepaji wa kodi hivyo kulazimika kuchukua hatua kali ikiwemo kuwasimamisha kazi vigogo kadhaa wa mamlaka hizo mbili.
Miongoni mwa vigogo ambao walianza kuonja chungu ya serikali ya Rais wa tano ni pamoja na Kamishna Mkuu wa Mamalaka ya Mapato Nchini (TRA), Rashed Badi aliyesimamishwa kazi pamoja na vigogo wengine saba walikamatwa na polisi akiwemo Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Tiagi Masamaki, kutokana na kutolewa kwa makontena 329 yaliyotoka bila ushuru.
Katika sakata hilo zaidi ya wafanyakazi 40 wa TRA walishikiliwa na Jeshi la Polisi kuhusina na tuhuma hizo ambazo zimeisababishia serikali hasara ya mabilioni ambapo pia Magufuli alivunja Bodi ya Mamlaka ya Bandari.
Mbali na kuvunja bodi hiyo, pia alitengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Profesa Joseph Msambichaka na kumsimamisha kazi Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Shaaban Mwinjaka kwa kushindwa kusimamia utendaji wa TRL na TPA.
Wengine waliokwisha kumbana na rungu la Rais Magufuli ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, ambaye ilielezwa kuwa Rais hakuridhishwa namna taasisi yake ikitekeleza majukumu na kushindwa kukabiliana na vitendo vya rushwa hususani kwenye upotevu wa mapato ya serikali katika bandari ya Dar es Salaam.
NIPASHE
Mbunge wa Jimbo la Mlalo wilayani Lushoto Mkoani Tanga (CCM) Rashid Shangazi amesema ataishauri serikali kufungua mpaka wa Tanzania na Kenya uliyopo Kivingo Kata ya Lunguza Wilayani Lushoto kwa lengo la kuwawezesha wakulima Jimbo hilo kuuza mazao yao nchi hiyo ya jirani.
Shangazi alisema kuwa suala la kero ya soko kwa wakulima wa Kata ya Lunguza ni kubwa na kwamba mazao ya kilimo ikiwemo mbogamboga yamekuwa tatizo kwa wakulima kuuza nchini Kenya ambapo kuna soko la uhakika.
Alisema kwa serikali kufungua mipaka hiyo ndio itakuwa njia pekee ya kuweza kuwapa soko la uhakika wakulima wa kilimo cha mbogamboga na mazao mengine Jimboni humo ili waweze kunufaika nacho kuliko ilivyokuwa sasa.
Hata hivyo Shangazi alibainisha kuwa sambamba na hilo kazi nyingine atakayoshughulikia ni ukarabati wa barabara ya kutoka Kata ya Mtae hadi Mnazi ambayo itaanza kwa njia ya changarawe ili kuhakikisha miundombinu inaimarika na kuweza kupitika nyakati zote.
“Naahidi kuhamasisha utalii kwenye Jimbo hilo kwa kutafuta
wawekezaji watakaoweza kujenga mahotel kutokana na Jimbo hilo kupakana na misitu ya asili na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ambayo itasaidia kutoa ajira kwa wananchi na kukuza pato lao na jamii kwa ujumla “alisema Shangazi.
Aidha pamoja na hayo aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuhakikisha wanashirikiana bega kwa bega ili kusukuma kasi ya maendeleo yao kwa kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili.
Akizungumzia namna atakavyoweza kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta ya Afya, Shangazi alisema atahakikisha anaongeza majengo ya vituo vya afya ili kuweza kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo za uchache wake.
Hata hivyo alisema mipango yake kwa vijana ni kuhakikisha kila kijiji kinapewa shilingi milioni 50 kupitia waratibu kata ili kuunda vikundi vya wajasiriamali 10-30 ili waweze kujiendeleza sambamba na kujikwamua kupitia uchumi wao.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyezahapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.