Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi. Maryprisca Mahundi, ameonesha kutoridhishwa na utendaji wa meneja wa shirika la Posta Mkoa Mara.
Naibu Waziri huyo akiwa ziarani wilayani Bunda Mkoani Mara, imemlazimu kuhoji utayari wa meneja huyo katika swala la kuwahudumia wananchi kwa viwango vinavyohitajika, huku akimtaka kujitafakari endapo bado anastahili kusalia kwenye hiyo nafasi au viatu vinampwaya.
Mhandisi. Mahundi ameendelea kusisitiza kuwa Serikali inataka kuona uwajibikaji wa kila mtumishi kwenye eneo lake kwani wameaminiwa kutoa huduma muhimu ya mawasiliano kwa wananchi.
Katika kuhitimisha ziara yake kwenye mikoa ya Mwanza na Mara, Naibu Waziri huyo amekagua baadhi ya minara iliyogharamiwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo kwenye shughuli za mkongo wa Taifa zilizopo kwenye Ofisi za Kampuni za Mawasiliano TTCL.