Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ametoa onyo kwa Makanisa na Misikiti nchini ambayo itashindwa kwenda kufanyiwa uhakiki itachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Waziri Lugola ameyazungumza hayo katika Mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Mwiseni, Kata ya Butimba, Jimboni kwake Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, akifafanua kuwa, uhakiki huo unalenga kuzifuatilia Taasisi hizo za dini kujua utendaji wake wa kazi unaendana na sheria za usajili.
Pia Waziri Lugola, amesema anajua kuna kero ya kusajili simu kutokana na upatikanaji wa vitambulisho vya taifa, lakini kutokana na upungufu huo amewaelekeza Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kutoa namba ili waweze wananchi kuweza kuendelea na usajili na pia amewataka NIDA wampee takwimu za Wilaya zote ili kujua ukubwa wa tatizo la usajili wa vitambulisho hivyo.
Lugola ameongeza kuwa, hakuna mwananchi atakayekosa kitambulisho cha taifa, na NIDA itawafuata mahali popote walipo nchini.