Leo July 4, 2018 Wafanyabiashara 2 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wa kupatikana na madini ya vito yenye thamani ya USD 1, 795,687.87 bila kuwa na vibali.
Washtakiwa hao ni Aazam Uddin Nazim na Ango Mbossa au Angomwile Mwamafupa au Emmanuel Angomwile.
Kwa pamoja washtakiwa wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Augustine Rwizile na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi.
Kishenyi amewasomea washtakiwa hao mashtaka matatu ya kula njama, kuongoza genge la uhalifu na kupatikana na madini ya vito bila ya kuwa na vibali.
Katika kosa la kwanza, wanadaiwa kati ya tarehe tofauti kati ya January mosi, 2017 na June 24, 2018 maeneo tofauti katika jiji na mkoa wa Dar es Salaam na nchini India walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la kuongoza genge la uhalifu.
Wanadaiwa katika kipindi hicho na maeneo hayo wakiwa sio watumishi wa umma lakini kwa kushirikiana na watumishi wa umma ambao hawajakamatwa kwa nia ovu na huku wakijua walipanga na kuratibu shughuli za genge la uhalifu kwa nia ya kupata faida.
Pia wanadaiwa June 3, 2018 maeneo ya Msisiri ‘A’, Mwananyamala, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, kwa pamoja walikutwa na madini ya vito yenye uzito wa kilogramu 75,957.30 yakiwa na thamani ya Dola za Marekani 1,795,687.87 (sawa n Bilioni nne) bila kuwa na vibali wala leseni.
Washtakiwa hao ambao wanatetewa na mawakili Hudson Ndusyepo na Derick Kaidi, hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Upande wa mashtaka umedai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo.
Hakimu Rwizile ameahirisha shauri hilo hadi July 18, 2018 kwa kutajwa na washtakiwa walirudishwa mahabusu.
Prof. Mbarawa baada ya kupewa Wizara ya Maji hivi ndivyo alivyotinga DAWASCO