Leo August 2,2018 tunayo stori kutokea Mahakamani Kisutu ambapo Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ameonya tabia ya washtakiwa kumpigia simu kuhusu masuala ya kesi akiwa nyumbani.
Hakimu Mashauri ameyasema hayo katika kesi ya kufanya maandamano yasiyo halali inayowakabili Viongozi 9 wa CHADEMA akiwemo Freeman Mbowe.
Hatua ya Hakimu Mashauri kutoa onyo hilo ni baada ya kumuhoji mdhamini wa mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko ambaye hakufika mahakamani kwa madai amepigiwa simu ya dharura kwenda shuleni kwa mwanaye nchini Kenya.
Hakimu Mashauri amesema kuna mshtakiwa alimpigia simu akiwa nyumbani, hivyo mdhamini anatakiwa kujua sababu ya mshtakiwa kutokuwa mahakamani.
“Ninapokuwa nyumbani mimi ni Mashauri, suala la kunipigia simu kuhusiana na mambo ya kesi siyo sahihi.” Hakimu Mashauri
“Mambo yanayohusu mahakamani yaishie mahakamani na siyo nikiwa nyumbani kwenye masuala ya kifamilia,” amesema Mashauri.
Baada ya kueleza hayo ameahirisha kesi hiyo hadi August 6,2018.
Awali upande wa mashtaka kupitia Wakili Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi ulidai kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali kutokana na Matiko kutokuwepo mahakamani wanaomba ahirisho.
Kwa upande wa Wakili Kibatala alidai mshtakiwa Matiko hayupo alipigiwa simu ya dharura kwenda Kenya shuleni kwa mwanae.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Katibu mkuu wa CHADEMA, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.
Miongoni mwa mashtaka yanayomkabili washitakiwa hao ni kula njama kwa nia ya kutenda kosa, kufanya mkusanyiko usio halali, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kukiuka tamko la kutawanyika na kuendeleza mkusanyiko wenye ghasia.
Washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Februari mosi na 16, mwaka huu, Dar es Salaam kwa pamoja na ujumla wao walikula njama ya kutenda makosa ya kufanya mkusanyiko usiohalali, mkusanyiko wenye ghasia na kukiuka tamko la kutawanyika.
Mbowe na wenzake pia wanadaiwa Februari 16, mwaka huu, katika viwanja vya Buibui na barabara ya Mwananyamala na Kawawa, Kinondoni, wakiwa wamekusanyika kwa nia ya kutekeleza azma ya pamoja ya kuandamana hivyo kuwatia hofu wananchi kwamba kutakuwa na uvunjifu wa amani.
Pia wanadaiwa wakiwa na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani siku hiyo waliandamana isivyo halali wakiwa na lengo la kuvamia ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na kutokana na mkusanyiko huo wa ghasia walisababisha kifo cha Akwilina Akwiline na majeraha kwa askari H. 7856PC Fikiri na E6976 CPL Rahim Msangi.
Alivyofikishwa Mahakamani anaetuhumiwa kutoa rushwa ya Milioni 90 kwa Lukuvi
https://youtu.be/dF0bVmE1Kk0