Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji (World Investment Forum) limefunguliwa tarehe 22 Oktoba 2018 Geneva, Uswisi na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) Dkt. Mukisa Khitui na litaendelea mpaka October 26,2018.
Kauli mbiu ya kongamnao ni ‘Uwekezaji kwa maendeleo endelevu’ (investing for sustainable development) ambapo majadiliano yatajikita kwenye changamoto za uwekezaji katika mazingira mapya ya utandawazi na mapinduzi ya viwanda (Globalization and Industrialization).
Balozi Dkt. James Msekela (wa tatu kutoka kulia) na Mkuregenzi wa TIC Bw. Geoffrey Mwambe (wa ili kutoka kulia) wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa uwekezaji Geneva,Uswisi.
Kongamano hilo la aina yake huandaliwa kila baada ya miaka miwili na UNCTAD kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya Uwekezaji. Takribani washiriki zaidi ya 5,000 wanashiriki kutoka nchi 160 duniani ikiwemo Tanzania na ujumbe wake unaongozwa na Balozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa Geneva, Dkt. James Alex Msekela.
Washiriki wa kongamnao hilo ni kutoka katika nyanja mbalimbali za umma na sekta binafsi ikiwamo Wakuu wa nchi, Mawaziri Wakuu, Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi za Uwekezaji. Wengine ni Watendaji wa Makampuni ya Kimataifa na Ushirikiano wa Hisa, Wasimamizi wa Mifuko ya Fedha, Wakurugenzi Wakuu wa Mashirika ya Sekta Binafsi, Wataalam wa eneo la Uwekezaji wa Kimataifa,Wabunge,Wawakilishi wa Vyama vya Kiraia, Wasomi Maarufu, na vyombo vya Habari vya Kimataifa.
Rais wa Namibia akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Geoffrey Mwambe katika Banda la Tanzania kwenye kongamano la kimataifa la Uwekezaji
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kama mdau wa masuala ya uwekezaji nchini kinashiriki katika kongamano hili ambapo Mkurugenzi Mtendaji Geoffrey Mwambe atashiriki katika vipindi/midahalo na majadiliano mbalimbali kwa lengo la kuinadi Tanzania kuwa ni nchi bora ya kuwekeza Afrika kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo amani, uchumi imara unaokua kwa kasi, uwepo wa rasilimali, uwepo wa miundo mbinu na uongozi bora.
Vilevile kupitia mikutano hiyo Mwambe atanadi fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania katika sekta mbalimbali pamoja na kuelezea mazingira ya uwekezaji. Mwambe pia atatumia mwanya huo kupambanua zaidi namna ambavyo Tanzania wa sasa inafanya mapinduzi ya kiuchumi hususani kuendeleza viwanda ili kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
Ufunguzi wa kongamano la Kimataifa la Uwekezaji
Sambamba na kongamano hilo, Kituo kwa kushirikiana na Ubalozi kinaiwakilisha nchi katika maonesho ya uwekezaji (World Investment Village) kupitia banda la Tanzania ambapo takribani nchi arobaini zinashiriki.
Lengo la maonesho hayo ni kueleza washiriki wa kongamano hali ya uchumi wa nchi husika, majukumu ya taasisi inayosimamia masuala ya uwekezaji, sababu za kuwekeza katika nchi husika, fursa za uwekezaji zilizopo, na namna ambavyo wawekezaji wanasaidiwa kuanzisha uwekezaji wao nchini.
Vilevile maonesho hayo ni njia pekee inayotoa fursa kwa nchi washiriki kujifunza mbinu/mikakati na kubadilishan auzoefu katika kuvutia uwekezaji zaidi. Baadhi ya nchi zinazoshiriki maonesho hayo ni Rwanda, Namibia, Gaboni, Malawi, Nigeria, Burkina, Faso, Siera Leone, Madagascar, Botwasana, Zimbabwe, Kongo, Burundi, Cote Devour, Mauritius na Zambia.
Kuwepo kwa washiriki wengi kutoka katika nyanja mbalimbali kwenye maeneo ya uwekezaji, ni wazi kwamba Kituo kitajifunza mengi kuhusiana na masuala ya uwekezaji ambayo yatatumika kama chachu ya kuleta maboresho katika sekta ya uwekezaji nchini. Ni imani yetu kubwa kwamba ushiriki wa Kituo katika kongamano hili utakuwa wa manufaa makubwa si tu kwa Kituo bali pia kwa Taifa ikiwa ni pamoja na kutoa mapemdekezoya Kisera kuhusu masuala ya uwekezaji.