Leo December 17, 2018 Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imetoa notisi ya siku 28 kwa Shirika la Ndege la Fastjet kwa nia ya kusitisha shughuli za kampuni hiyo ndani ya Tanzania kwakuwa limepoteza sifa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari amesema Fastjet imekosa vigezo kwenye uthibitisho wa leseni yake na hawana ndege za kuendelea kusafirishia abiria.
“Hivi karibuni kuna mabadiliko yalitokea kwamba wamiliki wake wa Uingereza walisitisha utoaji wa fedha kwa shirika hilo na kuliuza kwa watanzania, baada ya mabadiliko hayo Shirika hili limeteteleka kwa kiasi kikubwa kwa uwezo wa kifedha na kuanza kushindwa kufikisha masharti ya kiwango cha cheti cha uthibitisho na masharti ya leseni biashara, Mamlaka inatoa notisi ya siku 28 ya nia ya kusitisha shughuli za Kampuni hiyo ndani ya Tanzania,”– Johari
Johari amesema kuwa baada ya mabadiliko kufanyika Mamlaka ya Usafiri wa Anga ilitaka Fastjet watoe andiko jipya litakalotafsiri nini kinaendelea ndani ya Kampuni hiyo jambo ambalo halikutekelezwa.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Usafiri wa Anga sura ya 80 na Kanuni zetu pamoja na Kanuni inayosimamia Mambo ya Uthibiti Uchumi maana yake ni kwamba shirika la FastJet limepoteza sifa ya uthibitisho, hawana ndege, wala hakuna ‘Acountable Manager'”.-Johari
KIKOKOTOO KIPYA CHA MAFAO SSRA YATOA UFAFANUZI WA KINA “MKUPUO ASILIMIA 25”