Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inakusudia kumfikisha Mahakamani Dodoma, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Jacob Paul Nyangusi, kwa tuhuma za kutaka rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake.
Akitoa taarifa mbele ya vyombo vya habari jijini Dodoma, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Sosthenes Kibwengo amesema Mhadhiri huyo msaidizi amefunguliwa kesi ya uhujumu uchumi, kwa kosa la kutaka rushwa ya ngono, kinyume na kifungu cha 25 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007, ikisomwa pamoja na aya ya 21 ya jedwali la kwanza la vifungu vya 57(1) na 60(2) vya sheria ya uhujumu uchumi, sura ya 200, marejeo ya mwaka 2002.
Pamoja na mambo mengine, taasisi hiyo ikishirikia na ofisi ya taifa ya mashitaka, itawafikisha mahakama ya mkoa wa Dodoma, aliyekuwa diwani wa Kata ya Ntyuka jijini Dodoma Bw. Theobald Maina, Afisa Mtendaji Kata ya Ntyuka Benedict Mazengo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kata ya Chimala Bw. Anderson Mwaluko, kwa makosa ya matumizi mabaya ya mamlaka na ubadhirifu.