Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Jerry Slaa, amekabidhi magari 16 yenye thamani ya zaidi ya Sh. Bilioni 2.079 yatakayosaidia kupunguza gharama za kukodi magari wakati wa utekelezaji Mradi wa Uboreshaji wa Miliki za ardhi (LTIP).
Akizungumza katika hafla hiyo ya iliyofanyika leo Februari 19,2024 katika mji wa kiserikali Mtumba jijini Dodoma,Waziri Slaa,amesema kuwa magari hayo yatasaidia kutekeleza mradi huo katika sekta ya ardhi.
Waziri Slaa amesema kuwa magari hayo 16 yatakwenda kusaidia kuharakisha utekelezaji wa mradi huo ambao umejikita katika kuboresha milki za ardhi mijini na vijijini.
“Mradi huu utakwenda kuwa suluhu kubwa katika sekta ya ardhi kwani utasaidia kupima pamoja na kupanga matumizi bora ya ardhi mijini na vijijini na kutoa hati miliki kwa wananchi”amesema Waziri Slaa
Aidha Waziri Slaa,amemuagiza mratibu wa mradi huo kuhakikisha kuwa magari hayo yanatumika kwa matumizi yaliyopangwa na sivyo vinginevyo.
‘’Magari haya yatumike kwa kazi za mradi wale wote watakao kabidhiwa magari haya wayatumie vizuri, wayatunze tusione magari haya yamebeba mkaa au kufanyika katika shughuli za harusi tungependa kuyaona yakifanya kazi ya Mradi ili mradi ukiisha tuyatumie katika wizara yetu kwenye majukumu mengine’’. amesisitiza
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amesema thamani ya gari moja ni takribani Mil. 129.9 za Tanzania na magari hayo ni sehemu ya magari 70 yatakayonunuliwa kwa msaada wa Benki ya Dunia.