Kesi ya jinai namba 117/2017 inayowakabili washtakiwa watatu akiwemo Mbunge wa Mbozi Pascal Haonga imeahirishwa kutolewa hukumu na hakimu Mfawidhi Nemes Chami wa Mahakama ya Hakimu mkazi Wilaya ya Mbozi mkoa wa Songwe.
Upande wa Jamhuri umewakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali Joseph Pande akisaidiwa na Baraka Mgaya. Washtakiwa Mbunge Pascal Haonga, Mwenyekiti wa Kitongoji Mashaka Mwampashi na Katibu wa Mbunge Wilfred Mwalusanya ambao kwa pamoja wanatetewa na Wakili Boniphace Mwabukusi.
Kwa pamoja washtakiwa wanashtakiwa kwa makosa matatu Augut 28 mwaka 2017 katika ukumbi wa ofisi za Mamlaka ya Mji wa Mlowo majira ya saa nane mchana.
Imedaiwa na upande wa mashtaka kwa pamoja waliwazuia Polisi kutekeleza majukumu yao , kufanya vurugu na kukataa kutoka nje ya ukumbi.
Akiahirisha kesi hiyo Hakimu Mfawidhi Nemes Chami amesema ameshindwa kutoa hukumu kutokana na majukumu mengi ya kimahakama pia uzito wa kesi yenyewe hivyo ameahirisha hadi August 10 mwaka huu.
Nje ya Mahakama Wakili Boniphace Mwabukusi amesema anaunga mkono uamuzi wa Mahakama ili kutenda haki kwa pande zote mbili. Naye Mbunge wa Tunduma Frank Mwakajoka amesema Mahakama ndiyo chombo huru ana imani itatenda haki.
Aidha Mbunge wa Viti maalumu Mbeya Sophia Mwakagenda amesema wapinzani wamekuwa wakikumbwa na kesi nyingi zisizo na msingi. Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Songwe Herode Jivava amewataka wanachama wake kuwa watulivu kusubiri uamuzi wa Mahakama.