Leo July 11, 2018 Mhasibu Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania, Simon Maganga amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na makosa 6 ikiwemo uhujumu uchumi wa kuisababishia Serikali hasara ya Sh.Milioni 55.6
Katika makosa hayo, mashtaka 4 ni matumizi mabaya ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, shtaka la ufujaji, ubadhilifu na uhujumu uchumi kusababisha hasara.
Akimsomea hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakili wa TAKUKURU, Maxi Ali amedai mshtakiwa ametenda makosa hayo kwa nyakati tofauti.
Miongoni mwa mashtaka hayo anadaiwa kati ya January Mosi, 2009 na December 31, 2010 katika ofisi ya Bodi ya Pamba Tanzania iliyopo Wilaya ya Ilala kwa cheo Mhasibu Mkuu, alimdanganya mwajiri wake kuwa alitumia vocha za kuwasilisha mbegu za Pamba msimu wa 2009/2010 akijaribu kuonesha kampuni ya Afrisian Ginning Ltd ilinunua mbegu za Pamba kilo 25,129,258k wakati akijua kuwa si kweli.
Pia alimdanganya tena mawajili wake kwamba alitumia vocha za kuwasilisha mbegu za Pamba msimu wa mwaka 2009/2010 akijaribu kuonesha kampuni ya Nyanza Cooperative Ltd ilinunua Kilo 3,708,998 za mbegu za Pamba wakati akijua si kweli.
Katika kosa jingine anadaiwa kutumia vocha za kuwasilisha mbegu za Pamba msimu wa mwaka 2009/2010 akijaribu kuonesha kampuni ya kampuni ya S&C Ginning Ltd ilinunua kilo 17,152,590 za mbegu za Pamba wakati akijua si kweli.
Pia anadaiwa kutumia vocha za kuwasilisha mbegu za Pamba msimu wa mwaka 2009/2010 akijaribu kuonesha kampuni ya kampuni ya Kahama Oil Mill Ltd ilinunua 16,326,038 za mbegu za Pamba wakati akijua si kweli.
Katika shtaka la tano anadaiwa, akiwa katika ofisi ya bodi ya Pamba Tanzania, alifanya ufujaji na ubadhilifu wa Shilingi Milioni 55,637,680.
Mshtakiwa Maganga anadaiwa kuwa kati ya January Mosi, 2009 na December 31,2010 kwa makusudi aliisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh.Mil 55,637,680.
Mshtakiwa amekana kujibu mashtaka hayo baada ya kuruhusiwa kujibu mashtaka hayo kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka DPP aliwasilisha kibali cha kuipa ridhaa mahakama hiyo kuisikiliza kesi hiyo.
Kufuatia kibali hicho, mahakama imemsomea mshtakiwa masharti ya dhamana ambapo imemtaka
Kuwa na wadhamini wakili kila mmoja akitakiwa kuwa na barua na nakala ya vitambulisho ambapo kila mmoja atatakiwa kusaini bondi ya Sh, Milioni 28.
Aidha mdhamini mmojawapo ametakiwa kuwasilisha fedha Sh. Milioni 28 ama hati ya Mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha pamoja na hati yake ya kusafilia.
Kesi imeahirishwa hadi July 24,2018.