Serikali ya Kenya imewataka wakuu wa vitengo vya Manunuzi na Uhasibu katika Wizara, idara, Wakala na Mashirika yote ya Umma kwenda likizo ya lazima ya mwezi mmoja ili kupisha uchunguzi mpya dhidi ya ufisadi uliofanyika.
Maafisa hao wanatakiwa pia kuchunguzwa juu ya mtindo wa maisha yao ambapo wanatakiwa kupeleka taarifa zao katika ofisi ya mkuu wa utumishi wa Umma katika jumba la Harambee kuhusu mali wanayomiliki, madeni waliyo nayo na kazi walizozifanya awali, ifikapo Ijumaa, June 8, 2018.
Hili linafuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta aliyotoa katika maadhimisho ya Siku ya Madaraka kwamba taifa lazima lichukue hatua ya juu zaidi katika vita vyake dhidi ya ufisadi.
Watatakiwa pia kupimwa kwa kifaa ambacho ni cha kubaini iwapo mtu anasema ukweli au anahadaa(Polygraph or Lie detector). Watakaobainika wanasema uongo baada ya kutumiwa kwa kifaa hicho watafutwa kazi
Imeelezwa kuwa Maafisa hao wataendelea kupokea mishahara yao kama kawaida kipindi hicho cha likizo lakini kabla ya kwenda likizo hiyo ya lazima wanatakiwa kukabithi kazi kwa Manaibu wao