Leo May 13, 2018 Wadau na washirika wa Sekta ya Ardhi nchini, wamesema licha ya kazi nzuri zinazofanywa katika sekta ya ardhi bado kuna changamoto zinazohitaji ufumbuzi za kimfumo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kampuni ya Mipango Miji na Vijiji, Renny Chiwa amesema kwa mujibu wa takwimu za wizara takribani asilimia 85 ya ardhi yote nchini haijapangwa wala kumilikishwa hati miliki.
Amesema kuwa wanapongeza jitihada za Rais John Magufuli ikiwemo kufanya mabadiliko ya kiutendaji yanayogusa sekta ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
“Uamuzi wa Rais wa kuhamishia usimamizi wa watalaam wa Ardhi kwa Katibu Mkuu wa wizara ya Ardhi utaimarisha usimamizi wa idara husika katika halmashauri zetu, pia yatarahisisha shughuli zinatekelezwa kwa viwango,” amesema Chiwa
Chiwa amesema kuwa licha ya kazi nzuri katika sekta ya Ardhi, ni ukweli kwamba kuna changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa kimfumo.
“Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Ardhi takribani asilimia 85 ya ardhi yote nchini bado hayajapangwa wala kumilikishwa kwa hati miliki, hivyo kuna kazi kubwa ya kufanya,” -Chiwa
Kutokana na hatua hiyo, Chiwa amesema ipo haja ya kufanyika utafiti na kuandaa mpango kabambe wa ardhi ya viwanda utakaotoa dira kwa nchi nzima.