Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekataa kutoa hati ya kumkamata Mbunge wa Singida Mashariki CHADEMA) Tundu Lissu ambaye anakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi katika gazeti la Mawio kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
Hatua hiyo inatokana na upande wa mashtaka kuiomba Mahakama itoe hati ya kumkamata Lissu kwa madai anaonekana akizunguka nje ya nchi.
Mbali ya Mahakama kukataa kutoa hati hiyo, pia imewaonya wadhamini wa mshtakiwa huyo ambao ni Ibrahim Ahmed na Robert Katula kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ya kufika mahakamani hapo kila tarehe ya kesi itakapotajwa.
Uamuzi huo wa mahakama ulifikiwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Wankyo Simon kuiomba mahakama itoe hati ya kumkamata Lissu kwa sababu anazunguka katika nchi mbalimbali kutoa mihadhara.
Wankyo alidai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na mara ya mwisho mahakama ilitoa amri ya kuwaita wadhamini wa mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo (Lissu) ili kuja kueleza afya ya mtuhumiwa huyo.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba alimuamuru mdhamini wa Lissu, Ahmed kuieleza mahakama taarifa ya mshtakiwa huyo ambapo alidai kuwa mshtakiwa huyo yupo nchini Ubelgiji kwa ajili ya matibabu na Machi 20, mwaka huu alifanyiwa oparesheni ya 23.
Aidha mdhamini huyo na mwenzake waliiomba mahakama msamaha kwa kushindwa kufika mahakamani na kuahidi kufika mahakamani hapo katika kila tarehe ya kesi hiyo itakapotajwa.
Baada ya maelezo ya wadhamini hao, Wakili Wankyo aliendelea kudai kuwa mshtakiwa wa nne (Lissu) amekuwa akizunguka katika nchini mbalimbali kutoa mihadhara na hayupo hospitali kama ilivyodaiwa na wadhamini hao hivyo kama itafaa anaiomba mahakama iamuru mshtakiwa huyo akamatwe.
Wakili wa Utetezi Peter Kibatala alidai kuwa hakuna haja ya upande wa Serikali kuyazungumza hayo kwa kuwa tayari wadhamini wameshaieleza mahakama alipo mshtakiwa wa nne.
Kibatala aliiomba mahakama ione ni busara kuwakumbusha wadhamini hao majukumu yao na anafikiri kuwa mshtakiwa wa nne akimaliza matibabu atakuja kuendelea na kesi hiyo.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba aliwaonya wadhamini na kuwataka watambue majukumu yao na kuyatekeleza ikiwemo ya kufika mahakamani katika kila tarehe ya kesi itakapotajwa na kubainisha kuwa wanamiezi nane hawajaonekana mahakamani hapo.
Pia Hakimu Simba alisema “Hati ya kumkamata mshtakiwa (Lissu) kwa sasa haiwezi kutolewa hivyo ombi la kumkamata mshtakiwa huyo linakataliwa” alisema Hakimu Simba.
Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 25, Mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Kesi hiyo ipo katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka, lakini imeshindwa kuendelea kutokana na mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo, ( Lissu ) kuwa nchini Ubeljiji kwa ajili ya matibabu.
Februari nne, mwaka huu Mahakama hiyo iliaamuru wadhamini wa Lissu kufika mahakamani hapo jana kueleza maendeleo ya afya ya Mbunge huyo.
Lissu na wenzake watatu katika mahakama hiyo wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi katika gazeti la Mawio kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
Mbali na Lissu washtakiwa wengine katika kesi hiyo Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.
Kwa pamoja washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’
Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13 ,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.
Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.