Mwanamuziki ambaye pia ni Mwanasiasa, Robert Kyagulanyi maarufu ‘Bobi Wine’ ameshtakiwa akidaiwa kuwa na nia ya kumkera, kumshtua au kumkejeli Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Shtaka hilo linahusishwa na tukio la August 2018 ambapo Bobi Wine alishutumiwa kuongoza maandamano sehemu ambayo gari la Rais Museveni lilipigwa mawe na Waandamanaji.
Bobi Wine ambaye ni Mbunge wa Kyadondo Mashariki tayari anakabiliwa na shtaka la uhaini na anaweza kufungwa kifungo cha maisha iwapo atapatikana na hatia.
Pamoja na kufunguliwa shtaka la uhaini Agosti 23, 2018 katika Mahakama ya Kijeshi baada ya kushikiliwa kwa muda mrefu huku akiteswa, ameendelea kuikosoa vikali Serikali ya Rais Museveni.
Katika hatua nyingine, Mbunge huyo ametangaza pia kuwa atawania Urais wa Uganda dhidi ya Rais Museveni katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2021.