Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi ya kumiliki mali za zaidi ya Sh.Bilioni 3.6 kinyume na kipato halali inayomkabili Mhasibu Mkuu wa TAKUKURU, Godfrey Gugai hadi August 28,2018 ili kuendelea na ushahidi.
Wakili wa Serikali, Peter Vitalis amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya usikilizwaji, lakini wakili wa utetezi amepata dharula hivyo anaomba iahirishwe.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba aliutaka upande wa mashtaka unafika na mashahidi 2 katika kesi hiyo ambapo ameahirisha hadi August 28,2018.
Mbali na Gugai, washtakiwa wengine, ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali.
Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali za zaidi ya Sh.Bilioni 3.6 kinyume na kipato chake, ambapo anadaiwa ametenda kosa hilo kati ya January 2005 na December 2015.